2013-02-20 10:37:59

Uchaguzi mkuu nchini Kenya kiwe ni kipimo cha ukomavu wa kidemokrasia na umoja wa Kitaifa!


Wananchi wa Kenya wanaendelea kuhimizwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ukweli na uwazi; mambo msingi yatakayowezesha kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013. Wanaharakati wa masuala ya kisiasa wanasema, kuna haja ya kuendeleza majadiliano na viongozi wa Serikali, Kidini, Wananchi pamoja na sekta binafsi ilikufanikisha uchaguzi mkuu katika misingi ya haki, amani na utulivu.

Lengo ni nchi ya Kenya kufanikisha uchaguzi mkuu, utakaoendeshwa katika misingi ya haki na amani, kwani watambua maafa makubwa yaliyojitokeza nchini humo mara baada ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2007/ 2008. Vyombo vya habari vinaendelea kuhimizwa kusaidia kuimarisha haki, amani na utulivu, kabla, wakati na mara baada ya uchaguzi mkuu.

Viongozi wakuu wanaowania madaraka wakati wa uchaguzi mkuu wameombwa na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanadumisha amani na utulivu. Watu wanataka kuona baada ya uchaguzi wananchi wote wa Kenya wakiwa wameungana na kushibana na kamwe chaguzi zisiwe ni chanzo cha machafuko na uvunjifu wa amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.