2013-02-20 07:44:33

Imani na maisha ya mwanadamu ni mada tete zitakazochambuliwa na mabingwa hivi karibuni!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Taasisi ya Kipapa kuhusu maisha, katika mkutano wake wa XIX (19) itajikita kuhusu imani na maisha ya mwanadamu. Mkutano huu unatarajiwa kuwashirikisha viongozi waandamizi kutoka katika Mabaraza ya Kipapa hapa Vatican. RealAudioMP3

Mkutano huu utafunguliwa rasmi hapo tarehe 22 Februari 2013 kwa tafakari ya kina itakayotolewa na kardinali Willem Eijk, atakayejikita katika Injili ya Uhai. Itakuwa ni nafasi kwa Askofu mkuu Gerhard Ludwig kuchambua kwa kina na mapana dhana ya maisha katika mawazo ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Mada nyingine tete zitakazojadiliwa na wajumbe mbali mbali wenye uzoefu na masuala ya maisha ni pamoja na: Utakatifu wa maisha kama kielelezo makini cha maadili; zawadi ya maisha katika Maandiko Matakatifu; Jinsi ambavyo Imani na Sayansi vinaweza kulinda na kudumisha zawadi ya maisha katika Karne ya 21.

Baada ya wawezeshaji wakuu kutoa mada hizi kwa kina na mapana, wajumbe watapata fursa ya kuzijadili na kuzipembua kwa kuoanisha maisha ya binadamu kadiri ya mwanga wa maisha ya Yesu. Wajumbe pia wataangalia uhusiano uliopo kati ya fadhila ya imani, matumaini na mapendo katika maisha ya mwanadamu. Itakuwa ni nafasi ya Professa Chris Gastmans kutoa mikakati inayopania kulinda na kudumisha zawadi ya maisha ya mwanadamu.

Hii ni changamoto kubwa kwa Imani na Sayansi kulinda na kutetea zawadi ya maisha. Wajumbe pia wataangalia maisha mintarafu tamaduni mbali mbali na mwelekeo wake katika masuala ya elimu, tafiti za kimaadili katika uwanja wa sayansi ya tiba ya mwanadamu.

Kwa maneno machache, tunaweza kusema kwamba, Mkutano mkuu wa Taasisi ya Kipapa kuhusu maisha unapania kuenzi utamaduni wa maisha ya mwanadamu, changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, ambako utamaduni wa kifo unaonekana kushika kasi ya ajabu katika maisha na vipaumbele vya Jamii nyingi.








All the contents on this site are copyrighted ©.