2013-02-20 07:54:52

Ibueni mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wenu!


Waziri Mkuu Mizengo Pinda wa Tanzania, ameuagiza mkoa mpya wa Simiyu kuibua miradi mikubwa ya kiuchumi ya kilimo na viwanda ili kuharakisha maendeleo ya mkoa huo badala ya kukazania kujenga majengo makubwa ya kisasa ya ofisi. Alikuwa akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kwenye ukumbi wa KKKT mjini Bariadi, makao makuu ya Simiyu, Jumanne Feb. 19, 2013) pamoja na kuhutubia mkutano wa hadhara uwanja wa Saba Saba na na kupokea ripoti ya mkoa, Jumatatu, tarehe 18 Februari 2013.

Simiyu, ambayo pamoja na Geita, Katavi na Njombe ni Mikoa mipya iliyoanzishwa hivi karibuni, inazalisha karibu asilimia 50 ya pamba yote nchini na ina ng’ombe wapatao Milioni 1.5 na watu wanaokadiriwa kufikia milioni 1.6. “Mnaweza kuzitumia fursa na rasilimali hizi kuleta maendeleo. Lakini mkikazania kujenga majengo makubwa na ya kisasa ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya, mtagundua baadaye kuwa hamjawasaidia hata kidogo wananchi wenu,” alisema.

Mkoa wa Simiyu ulianzishwa rasmi Machi, 2012 na pamoja na ile mingine mipya mitatu, inafanya idadi ya mikoa yote ya Tanzania Bara kuwa 25. Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali huanzisha maeneo mapya ya utawala kusogeza uongozi na utawala karibu na wananchi ili usimamiaji wa shughuli za maendeleo na huduma za jamii uwe na tija zaidi.

Pinda aliwaambia Wajumbe wa kikao hicho kuwa mkoa huo unaweza ukafanya sherehe za uzinduzi wake, lakini siyo kwa mbwembwe, ila utumie sherehe hizo kuwakaribisha wawekezaji binafsi waone fursa za kuwekeza katika mkoa huo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa, Mtemi Andrew Chenge, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, alisema maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu kwa Kamati hiyo ya maendeleo yatashughulikiwa kwa uzito wake wote. Baadaye alasiri, Waziri Mkuu alitembelea mnada wa ng’ombe na mnada wa vitu vya kawaida vya matumizi ya kila siku mjini Bariadi kujionea mwenyewe uendeshaji wa shughuli hizo na kuzungumza na wafanyabiashara, wachuuzi na wanunuzi.








All the contents on this site are copyrighted ©.