2013-02-20 09:15:13

Choko choko za uchinjaji wa kitoweo! Kila mtu ana haki ya kuamini katika imani yake, lakini haka mamlaka wala sheria ya kumlazimisha mtu mwingine kufuata miiko na ibada ya dini yake!


Wakati Watanzania bado wanaendelea kuomboleza kifo cha Padre Evarist Mushi aliyeuwawa kikatili Zanzibar wakati anakwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa limechomwa moto Zanzibar. Hili ni Kanisa la Siloam lililoko kwenye eneo la Kiyanga, Kisiwani Unguja.

Hadi sasa kuna jumla ya Makanisa 26 yaliyokwisha kuchomwa moto, lakini Jeshi la Polisi halijafanikiwa kuwatia mbaroni wahusika wa matukio yote ya unyanyasaji na mauaji ya viongozi wa kidini. Taarifa za Jeshi la Polisi zinabainisha kwamba, hizi ni hujuma dhidi ya Kanisa. RealAudioMP3

Watanzania wengi wanasema hizi ni njama za kuitumbukiza nchi katika machafuko ya kidini kwa kuendelea kuchochea chokochoko na uhasama wa kidini, jambo ambalo ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Wanaofanya vitendo hivi kamwe si "wahuni" kama ambavyo waliwahi kusema baadhi ya viongozi wa Serikali, bali ni kundi la magaidi wanaotaka kuonesha makucha yao na kuanika udhaifu wa Serikali katika kulinda raia na mali zao.

Machafuko ya kidini yaliyotokea kwenye Kitongoji cha Buselesele, Mkoani Geita na Nyehunge, Mkoani Mwanza ni viashilia vya tatizo kubwa linalofanyiwa mzaha nchini Tanzania. Katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kinzani za kidini mkoani Geita, chini ya harakati za Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ulishindikana kutokana na masharti ambayo yakipimwa kwa mizani ya haraka haraka mtu anaweza kusadikishwa kwamba, Serikali ya Tanzania ina wapendelea Wakristo.

Sharti la kwamba, watuhumiwa wanne wa mauaji ya Mchungaji Mathew Kachira waachiwe huru na wapewe haki ya kushiriki katika mkutano na Waziri mkuu ni jambo ambalo limewaacha watu wengi wakijiuliza kuhusu maana ya haki na utawala wa sheria.

Madai kwamba, wajane wa wale waliofariki dunia kwenye machimbo ya dhahabu Kahama pia watembelewe na kufarijiwa na Serikali linaleta usumbufu katika mawazo ya wengi. Katika machimbo watu wanakwenda kutafuta riziki; hapa ni masuala ya kiuchumi na dini haina uhusiano wowote ule!

Madai ya kuwatunza wajane wa mauaji yaliyotokea kuanzia Mwembechai kunako mwaka 1998 hadi leo hii yanaonesha chuki na uhasama wa kidini unavyoendelea kufichika mioyoni mwa watanzania. Hii inadhihirisha madai ya dhana ya "Mfumo wa Ukristo" kutawala nchini Tanzania, kinyume cha ukweli wa mambo!

Mchungaji Christopher Mtikila akihojiwa wakati wa mazishi ya Padre Evarist Mushi wa Jimbo la Zanzibar, Jumatano, tarehe 20 Februari 2013 anasema uvumilivu ni tunda la Roho Mtakatifu kwa Wakristo. Kwa Waislam wenye mapenzi mema wanatambua kwamba, Mkristo ni rafiki mwema. Jambo la msingi kwa sasa ni kuombea amani, utulivu, upendo na mshikamano. Ni wakati kwa watanzania kufikiria jinsi ya kung'oa mizizi na shina la fitina na choko choko za kidini badala ya kuangalia majani na matawi.

Askofu Damian Dallu wa Jimbo Katoliki Geita katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, kila dini na dhehebu lina utaratibu, kanuni na sheria zao katika kusimamia maisha ya waamini wake. Kamwe waamini wa dini na madhehebu mengine wasifungwe na taratibu, kanuni na sheria hizi. Serikali isimamie na kuratibu uhuru wa kidini na kamwe Serikali haina mamlaka kisheria wala kikatiba kushurutisha waamini wa dini nyingine kufuata masharti na kanuni za dini moja. Huu ni uhuru wa mtu binafsi.

Askofu Dallu anasema, kama mtu anachinja kitoweo kwa ibada ya dini yake, asimlazimishe mtu mwingine kufuata Ibada hii, kwani Serikali haina dini, lakini wananchi wana dini na imani zao zinazopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Dini na imani ya kweli itasimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai bila kujikita katika tofauti za kidini, kikabila au mahali anapotoka mtu! Dini iwe ni mvuto kwa watu wengine; iwe ni mahali pa kutetea na kujenga: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anayo haki ya kuishi. Watu wathaminiane na kuheshimiana kutoka na tofauti zao ili kukamilishana.

Askofu Damian Dallu anabaianisha kwamba, nchi ya Tanzania inaundwa na: watu wanaoamini katika dini za jadi, Waislam na Wakristo. Hata wale wanao amini dini za jadi wana haki ya kuishi na kufaidi matunda ya uhuru nchini Tanzania. Wakristo na Wasilam wasidhani kwamba, Tanzania ni kwa ajili ya waamini wa dini hizi mbili tu na hivyo kujenga kiburi cha kuwasahau na kuwatenga watanzania ambao bado wanaamini katika dini za jadi.

Watanzania wote wapaswa kushirikishwa katika fursa na mchakato wa kutafuta mafao ya wengi; kwa kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Watu waheshimiane na kuthaminiana; wakubali tofauti zao na kujitahidi kukamilishana! Ubabe hauna tija, mafao wala maendeleo kwa watanzania wengi!









All the contents on this site are copyrighted ©.