SECAM -yatoa barua ya kichungaji juu ya Utawala kwa viongozi wa Afrika.
Maaskofu Katoliki wanachama wa SECAM, chombo kinachounganisha Mabaraza ya Mabaraza
la Maaskofu Barani Afrika na Madagascar, wametoa barua yao ya kichungaji kwa viongozi
wa Afrika, juu ya utawala bora, na kwa ajili ya ufanikishaji mazuri kwa wote katika
kipindi cha mpito kuelekea demokrasia Afrika.
Barua hiyo ni wito kwa viongozi
wa kisiasa , kutenda kwa haki kwa ajili ya kuijenga jamii ya Afrika iliyo bora zaidi
na siyo tu kwa manufaa ya wasomi bali raia wote. Maaskofu wametoa barua hiyo ya
kurasa 16, kama matokeo ya kukamilika kwa Mkutano wao wa hivi karibuni mjini Accra.
Barua iliyotiwa sahihi na Rais wa SECAM, Kardinali Plycarp Pengo , Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Maaskofu wanawasisitiza viongozi wa Afrika kukataa
utendaji wowote ule, unaolenga kuvuruga matokeo halali ya chaguzi kuu na kila aina
ya uozo na ufisadi, badala yake, waweke kipaumbele cha kwanza, mipango ya kufuta
ufukara. Aidha viongozi wa Afrika ni lazima wahakikishe uwepo wa utaratibu katika
miliki na mgao mzuri wa maliasili ya Bara la la Afrika, ili maliasili iwe ni kwa manufaa
watu wote.
Askofu Mkuu Gabriel Mbilingi wa Jimbo Kuu la Lubango Angola, ambaye
pia ni Makamu wa Rais wa Secam, akirejea barua hiyo, juu ya utawala: kwa ajili ya
mazuri kwa wote na demokrasia barani Afrika , ameeleza kwa kifupi yaliyomo kwamba,
ni utetezi wa mazuri na heshima kwa haki za binadamu na ukuzaji wa utawala bora kama
kipingere muhimu cha Kiinjili. Na kwamba Kanisa ni wajibu wake kusimiamia amani
katika mapito ya kisasa barani Afrika, kwa ajili ya uaptikanaji wa uhuru , maridhiano
na ukarabati wa kweli. Kanisa pia linaunga mkono maamuzi yanayolenga kuheshimu utu
wa binadamu na ushiriki wake katika maamuzi yanayoleta usawa na mwelekeo mzuri wa
ustawi wa maisha ya wana wa Afrika. Na kwamba, barua hii, ni uvuvio kutoka hati
ya Kipapa ya "Africae Munis", iliyotolewa kama matokeo ya Sinodi ya Maaskofu ya Pili
kwa Afrika, vipengere namba 23 hadi 29 vya hati hiyo, ambamo kwa kifupi mnaelezwa
kwamba amani si tu zawadi ya kupokea lakini ni uwajibikaji katika utendaji wa kujenga
amani ya kweli, kama sharti la lazima, kuwa na ufahamu wakutosha katika uvumilivu,
huruma, mshikamano na udugu ndani ya jumuiya na jamii kwa ujumla. Ni muhimu kujali
kuinua utambuzi katika ngazi za kitaifa na kimataifa, na kutafuta mfumo unaofaa kwa
ajili ya mgao wa utajiri wa maliasili na ukuzaji wa ushirikiano kwa ajili ya maendeleo
na katika kupata majawabu yanayofaa wakati kunapotokea kutokuelewana. Utume wa
SECAM, hulenga kulikuza Kanisa kama familia ya Mungu barani Afrika , kudumisha na
kukuza mawasiliano , ushirikiano na kutenda kwa pamoja kama Baraza la Maaskofu Katoliki
Afrika . Na pia kuendeleza ushirikiano na serikali na taasisi zingine katika mwingiliano
wa Maendeleo ya watu wa Afrika.