Professa Mario Monti akutana na Papa Benedikto XVI
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, jioni tarehe 16 Februari 2013
amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Professa Mario Monti, Waziri mkuu wa
Italia. Hili lilikuwa ni tukio la Baba Mtakatifu kuagana rasmi na Professa Monti.
Taarifa kutokana katika mkutano huu zinabainisha kwamba, mazungumzo ya viongozi hawa
yamefanyika katika hali ya utulivu na amani ya ndani.
Professa Monti kwa mara
nyingine tena amemshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutokana na upendo
na heshima kubwa aliyowaonesha wananchi wa Italia katika kipindi chote cha uongozi
wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa, itaendelea kukumbuka
na kuenzi mchango wake mkubwa katika maisha ya kiroho, kimaadili na utu wema.
Professa
Monti anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni kiongozi aliyeguswa kwa
namna ya pekee na mahangaiko ya watu: kiroho, kimwili na kijamii. Licha ya magumu
na kukengeuka kwa utu na maadili mema, bado Baba Mtakatifu anaonesha matumaini yake
ya dhati kwa wananchi wa Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake.