Hali ni tete Zanzibar! Kuna ubaguzi na unyanyasaji wa kidini!
Kutokana na mfululizo wa matukio ya uchomaji moto wa Makanisa, madhulumu na hatimaye
mauaji ya viongozi wa Kanisa, sasa ni uhakika na wala hakuna siri tena kwamba, kuna
madhulumu ya kidini Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Watu wanaishi kwa vitisho na
hofu kutokana na imani yao, kiasi kwamba, ule uhuru wa kuabudu kwa sasa uko mashakani.
Huu ni udhaifu
mkubwa ambao unaoneshwa na Serikali ya Tanzania kwa wakati huu, hata baada ya kusherehekea
Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa bendera.
Hayo yamesemwa na Askofu Damian Dallu
wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican. Anasema,
jaribio la mauaji ya Padre Ambrose Mkenda ni kielelezo cha wazi kabisa cha kinzani
na choko choko za kidini. Hili ni tukio ambalo lilipangwa na alama za nyakati zinabainisha
hayo kutokana na kuzagaa kwa vipeperushi, CD na DVD zenye kashfa na maneno ya uchochezi
dhidi ya Wakristo.
Hatua inayofuata kwa sasa mauaji ya viongozi wa Kanisa na
dalili za utekelezaji wa mikakati hii zinaanza kujionesha. Watanzania wakumbuke kwamba,
amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomwajibisha pia binadamu. Askofu Dallu
anawahimiza Wakristo, Waislam na Watanzania wote wenye mapenzi mema kuendelea kushikamana
kwa dhati kulinda na kutetea: haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; vikundi
vinavyotaka kuvuruga amani ni watu wachache sana, ikilinganishwa na umati mkubwa wa
watanzania wanaotaka kuendeleza mshikamano pamoja na kuheshimiana.
Kwa Wakristo
hiki ni kipindi cha ushuhuda wa imani. Maaskofu Katoliki wamepokea kwa mshtuko mkubwa
mauaji ya Padre Evaristi Mushi wa Jimbo Katoliki Zanzibar. Ni mauaji ya kikatili yaliyofanywa
wakati anakwenda kutekeleza wajibu na utume wake kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa,
ili kuombea: upendo, haki na amani. Kwa hakika, Zanzibar kuna unyanyasaji na ubaguzi
wa kidini. Vikundi vinavyochochea chuki, uhasama na machafuko ya kidini vinajulikana,
lakini Serikali inaendelea kuwafumbia macho.
Askofu Damiani Dallu anasema,
Kanisa halitashangaa kuona kwamba, matukio kama haya ya madhulumu na mauaji ya viongozi
wa Kanisa yatafuata. Lakini jambo la msingi kwa watanzania na watu wote wenye mapenzi
mema kukumbuka ni kwamba, vita haina macho! Kila mtu ajifunge kibwebwe kudumisha misingi
ya: haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Wasikubali kutumiwa na baadhi
ya watu kuleta choko choko na ubaguzi wa kidini. Wananchi wajitahidi kusoma alama
za nyakati, ili kuwachagua viongozi watakaotetea mafao ya wengi, umoja na mshikamano
wa kitaifa!