Watu wasiokuwa na makazi Msumbiji wananyemelewa pia na ugonjwa wa Kipindu pindu!
Hofu imetanda Kaskazini mwa Msumbiji, kutokana na kulipuka kwa ugonjwa wa Kipindu
pindu na kwamba, hadi sasa kuna watu zaidi ya mia tatu ambao wamekumbwa na ugonjwa
huo, katika eneo la Capo Delgado. Taarifa zinasema, Pemba ina idadi kubwa ya wagonjwa
wa Kipindu pindu.
Hii ni kutokana na mazingira machafu pamoja na athari za
mafuriko yaliyopelekea kubomoka kwa vyoo vingi katika maeneo yaliyokumbwa mafuriko,
kadiri ya taarifa zilizotolewa na Bibi Lidia Chongo, afisa mwandamizi wa Afya nchini
Msumbiji. Kuna vituo vitano vilivyotengwa ili kutoa huduma kwa wagonjwa wa Kipindu
pindu nchini Msumbiji. Kuna idadi kubwa ya wananchi wa Msumbiji ambao makazi yao yalibomolewa
kutokana na mafuriko yaliyotokea kwenye Mto Lipopo hivi karibuni.
Mashirika
ya Misaada ya Umoja wa Mataifa, yanaomba kiasi cha dolla za Kimarekani Millioni 30.6
ili kuwahudumia waathirika wa mafuriko nchini Msumbiji pamoja na kuanza mchakato wa
ujenzi wa nyumba na miundo mbinu iliyoharibiwa kutokana na mafuriko hayo.