2013-02-18 15:01:11

Papa aanza wiki moja moja ya mafungo ya kwaresima


Jumapili jioni , 17 Februari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto XV1, akiwa pamoja na wasaidizi wake katika jengo la Kipapa na wafanyakazi katika ofisi za Curia ya Roma, walianza mafungo yao ya wiki moja ya kipindi cha kwaresima, kwa Ibada ya Masifu iliyofanyika katika Kikanisa cha Mama wa Mkombozi cha Mjini Vatican .
Mafungo haya yatakayo kamilika Jumamosi 23 Februari, yanaongozwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Utamaduni. Mafungo yanaongozwa na Madambiu : Sura ya Mungu na Sura ya muumini katika Maombi.
Kardinali Ravasi , akitoa tafakari yake ya kwanza, alianza kwa kurejea maamuzi ya Papa Benedikto XV1, kustaafu KIti cha Petro, kwa mtazamo wa sura ya Kibiblia, akimfananisha na Musa alivyo waacha wana wa Israel na kupanda mlimani kusali, wakati wana wa Israel, wakipambana na Wamaleki.

Kardinali Ravasi, amekitaja kitendo la kuamua kustaafu, kuwa ni maamuzi ya mtu shupavu na muhimu kwa Kanisa, katika maana kuingilia kati kwa kina, kama alivyofanya Musa, alijitenga katika upweke wa sala mlimani na kuwaacha watu wake bondeni wakipambana , vivyo hivyo Benedikto XV1, analicha kanisa chini wake bondeni , ambapo kuna Wamaleki. Vivyohivyo Papa anakwenda pembeni katiak upweke wa sala na kuwacha watu wake katika bonde na vumbi la maovu, hofu, vitisho na majinamizi mengi, lakini pia kuna tumaini.

Papa Benedikto XV1, Yeye sasa baada ya kipindi cha miaka nane cha kuliongoza Kanisa, analiacha, waamini wakiwa na utambuzi kwamba, anakwenda mlimani kusali zaidi kwa ajili Kanisa.

Kardinali kisha alitoa mwaliko wa kujiunga katika tafakari hii ya kwanza kwa ukimya katika nafsi, ukimya wa kujiweka huru dhdi ya kelele nyingi za harakati za maisha ya kila siku.

Aidha ameutaja wakati huu wa mafungo, pia kuwa ni wakati muafaka kwetu sote, kujiweka huru kiroho na mambo ya kidunia , huru dhidi ya matope ya dhambi, huru dhidi ya uzushi na upupu wa maneno, hasa katika siku hizi, ambamo masikio yanateswa na maneno mengi ya uzushi.

Na ameitafakari sala ya mzaburi , katika mwanga wa imani kwamba, kusali ni kupumua, kwa kuwa sala ni hewa kwa maisha yetu; kusali ni kufikiri, kusali ni kumjua Mungu, kama alivyofanya Maria, aliyaweka yote ndani ya moyo wake. Sala pia ni kukabiliana na Mungu, hasa wakati tunapokuwa tumekaukiwa kiimani, na kuingizwa katika giza la vishawishi vya maisha. Kusali ni kuinua kilio cha kukata tamaa na hali za kutaka hata kukufuru. Hivyo basi, kusali, inakuwa ni upendo, unaotuwezesha kukumbatiwa na Mungu. Na sala ni wakati wa wapenzi wawili wapendanao, muumini na Mungu, kutupiana jicho katika hali ya ukimya.

Kardinali alihitimisha tafakari yake ya kwanza, kwa kuwarejesha katika ukimya wa fumbo la Kuu la Pasaka akisema , katika Imani , kama ilivyo katika upendo , ukimya huwa ni fasihi zaidi ya maneno. Ni mambo mawili yanarandana, kwani pale moja linapokosekana, yote hukosa mweleko na mara hutoweka.








All the contents on this site are copyrighted ©.