2013-02-18 09:04:53

Jubilee ya miaka 25 ya Baraza la Maaskofu Katoliki India: waliko wa kushikamana katika maisha na utume wa Kanisa


Baraza la Maaskofu Katoliki India, hivi karibuni limeadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu lilipozinduliwa sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kipindi chote hiki kimekuwa ni fursa ya kuku ana kukomaa kwa kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinajitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, Umoja na Mshikamano wa dhati. Ni matumaini ya Watu wa Mungu kwamba, Maaskofu wao mahalia watawashirikisha kwa kina man’gamuzi ya Imani, Matumaini na Mapendo, kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili.

Wanatamani kuwaona Maaskofu wachapakazi, wakiwa na ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitoa kimaso maso kumtangaza Kristo kwa ushupavu na moyo mkuu. Askofu hana budi kuwa ni kiungo thabiti katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuwawezesha Makleri na Waamini Walei kushirikiana kwa pamoja katika kutangaza Injili ya Kristo sanjari na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Maaskofu daima wakumbuke kwamba, Kanisa ni la Kristo mwenyewe, amewadhaminisha: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu. Watu wanataka kuona mifano bora kutoka kwa viongozi wao.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Barza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini India, kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki India lilipoanzishwa. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kujenga na kuimarisha uhusiano wao wa dhati na Kristo kwa njia ya Sala na kwa njia hii wanaweza kuwa kweli ni vyombo madhubuti vya Uinjilishaji, katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Maaskofu wajitahidi kutafuta fadhila ya hekima katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao ndani ya Kanisa bila kusahau kuomba ushauri kwa masuala mbali mbali. Maaskofu wawe na nguvu katika kutafuta mema na kuyaendeleza; wawe na ujasiri wa kukabiliana na madhulumu, mateso hadi kifo, daima wakijitahidi kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Kristo, utu na heshima ya binadamu. Ukweli, uwazi na haki viwawezeshe Maaskofu kuwa kweli ni viongozi wa Kanisa kwa kuondokana na kinzani zisizokuwa na msingi; majungu na hata wakatimwingine upendeleo kwa baadhi ya watu.

Maaskofu wasimame kidete kulinda na kutetea Imani ya Kanisa Katoliki. Kwa kuwa ni Walimu, wajitahidi kurithisha Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Liturujia na Mapokeo ya Kanisa, daima wakijitahidi kuwa na uchaji wa Mungu. Wayafahamu Maandiko Matakatifu kwa kina na mapana, wawasaidie waamini wao kumfahamu Yesu, ili waweze kupata uzima wa milele. Maandiko Matakatifu yasomwe na kutafsiriwa mintarafu Mafundisho Tanzu pamoja na Mapokeo ya Kanisa. Majando kasisi wanapokuwa katika malezi, wapewe mafundisho sahihi kuhusu falsafa na taalimungu.

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kanisa pia linaadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Waraka wa Kichungaji kuhusu Waamini Walei, ”Christifideles Laici”. Hili ni kundi muhimu sana katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Watambue kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Maaskofu wajitahidi kuimarisha na kushirikisha vyama vya kitume kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kwani hivi ni zawadi ya Roho Mtakatifu, lakini jambo la msingi pia ni kudumisha umoja na mshikamano wa Familia ya Mungu katika Kanisa Mahalia. Maaskofu ni kielelezo cha umoja wa Kanisa na kwamba, wanayo dhamana ya Kuinjilisha ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Mapadre ni wasaidizi wa kwanza wa Maaskofu katika utume wao! Ni wajibu na dhamana kubwa kwa Maaskofu kuwa karibu na Mapadre pamoja na watawa wanaofanya nao utume. Wawajali katika maisha na mahangaiko yao ya ndani kwa kuwasaidia kadiri ya uwezo wa Maaskofu. Upendo, umoja na mshikamano uwe ni dira katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Jubilee ya miaka 25 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki India lilipoanzishwa, iwe ni fursa ya kufanya tafakari ili kubainisha mafanikio, mapungufu na kujiwekea malengo kwa siku za usoni.








All the contents on this site are copyrighted ©.