Wakili Ernst Von Freyberg ateuliwa kuwa Rais wa Benki ya Vatican
Tume ya Makardinali inayosimamia na kuongoza Benki ya shughuli za kidini mjini Vatican,
IOR, kwa kuzingatia sheria na kanuni za Benki hii imemteuwa Wakili Ernst Von Freyberg
mwenye umri wa miaka 55 kuwa Rais wa Benki ya Vatican na wajumbe wengine wanne wa
Bodi wataendelea na nyadhifa zao kama kawaida. Uteuzi huu umeridhiwa na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita.
Mchakato na hatimaye, uteuzi wa Rais wa Benki ya
Vatican umefanywa kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia vigezo vya: maadili, sheria,
ukweli, uwazi, tija, ufanisi na weledi, kama alivyobainisha Padre Federico Lombardi,
msemaji mkuu wa Vatican, wakati akizungumza na waandishi wa Habari mjini Vatican.
Mchakato huu umefanywa na Wakala wa kimataifa anayejitegemea kwa kuwasilisha majina
kadhaa na hatimaye jina la Wakili Ernst likateuliwa. Ni mtu mwenye uzoefu mkubwa katika
shughuli za Kibenki na masuala ya Kanisa.