2013-02-16 14:05:09

Rais Otto Fernando Perez Molina akutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mjini Vatican


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, tarehe 16 Februari 2013 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Otto Fernando Pèrez Molina wa Guatemala na baadaye akakutana na viongozi waandamizi kutoka Vatican chini ya Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao wameridhika na uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Guatemala.

Rais Molina amelipongeza Kanisa Katoliki kutokana na mchango wake katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini mwake, hususan katika sekta ya elimu na urithishaji wa tunu msingi za kiutu na kiroho, bila kusahau huduma za kijamii kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Rais amelishukuru Kanisa kwa mchango mkubwa lililotoa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lililoikumba Guatemala hivi karibuni.

Viongozi hawa wawili wameonesha umuhimu wa pande hizi mbili kuendelea kushirikiana katika harakati za kupambana na umaskini; udhibiti wa matumizi haramu ya dawa za kulevya; vitendo vya jinai na huduma kwa wageni na wahamiaji. Wamekubaliana kimsingi kwamba, maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa na kudumishwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.