2013-02-16 12:00:26

Mh. Padre Titus Joseph Mdoe, ateuliwa na Papa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Mheshimiwa Padre Titus Joseph Mdoe kutoka Jimbo Katoliki Tanga, kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Mdoe alikuwa ni Makamu wa Chuo Kikuu kishiriki cha Stella Maris, Kituo cha Mtwara.

Askofu mteule Titus Joseph Mdoe alizaliwa kunako tarehe 19 Machi 1961, Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga. Akapata masomo yake ya msingi, Kongei, Tanga na baadaye akapelekwa kuendelea na masomo Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, iliyoko Jimbo Katoliki, Morogoro. Kwa masomo ya Falsafa alipelekwa Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki Moshi. Akafundwa kwa masomo ya Taalimungu, Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Baada ya majiundo na masomo yake ya Kipadre, akapadrishwa kunako tarehe 24 Juni 1986 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga. Tangu wakati huo ametekeleza majukumu yake kama Paroko msaidizi Gare, Mkurugenzi wa miito Jimbo Katoliki Tanga. Amefanya utume pia kama Paroko msaidizi Kanisa kuu la Mtakatifu Anthoni Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2000 alikuwa ni Paroko wa Hale. Mwaka 2000 hadi Mwaka 2008 alikuwa ni Paroko wa Kanisa kuu la Mtakatifu Theresa.

Kuanzia Mwaka 2008 hadi Mwaka 2010 akapelekwa kujiendeleza kwa masomo ya juu Chuo Kikuu cha St. Clara University, Calfonia, USA, ambako alijipatia shahada ya uzamili katika shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho. Kunako Mwaka 2010 akarejea Tanzania kuendelea na shughuli zake za kichungaji na kupangiwa kuwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu kishiriki cha Stella Maris, Kituo cha Mtwara, kilichoko Jimbo Katoliki la Mtwara, hadi kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Askofu Msaidizi, Jimbo kuu la Dar Es Salaam.







All the contents on this site are copyrighted ©.