2013-02-16 07:26:08

Imani na upendo ni chanda na pete!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa, tarehe 15 Februari 2013 alikutana na wanachama wa Chama cha shughuli za Mtakatifu Petro, kwa mara nyingine tena, amekazia umuhimu wa fadhila ya imani inayopaswa kuuishwa kwa njia ya matendo. Ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuifanyia kazi fadhila hii, ili hatimaye, iweze kukua, kukomaa na kuzaa matunda yanayotarajiwa na kwamba, kuna uhusiano wa dhati kati ya imani na mapendo.

Baba Mtakatifu amewakumbusha wanachama hao kwamba, imani na mapendo ni chanda na pete na kamwe fadhila hizi haziwezi kutenganishwa, bali imani inapaswa kuoneshwa kwa njia ya matendo ya huruma. Hiki ni kielelezo makini cha imani tendaji, imani inayojikita katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Huduma za kimwili zinazotolewa na Kanisa ni dhamana fungamanishi inayopania kuwashirikisha watu ule upendo wa Kristo ambao Kanisa limeupokea na kuwagawia wengine.

Hii ni changamoto inayotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa kuwataka waamini kuhakikisha kwamba, waamini wanakutana na Kristo anayewaletea mabadiliko katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili hatimaye, kutolea ushuhuda wa maana ya upendo wa Kikristo. Matendo ya huruma wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima ni hatua inayomwezesha mwamini kumwendea Kristo na Kristo kumwendea mwanadamu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawatakia wanachama wa Chama cha shughuli za Mtakatifu Petro, kuendelea kuimarika wanapofanya hija yao ya kiroho kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro. Iwe ni fursa ya kukuza na kuimarisha neema ya ubatizo, daima wawe na ari na moyo wa kutaka kutolea ushuhuda wa imani tendaji katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Wanachama hawa kwa upande wao, wamemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wataendelea kuchangia kwa hali na mali shughuli za matendo ya huruma zinazofanywa na Khalifa wa Matakatifu Petro, kama kielelezo cha upendo na mshikamano unaoonesha ile furaha ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa njia ya imani wanaweza kuwaonjesha jirani zao maskini na wahitaji ile sura ya Kristo mfufuka.

Ndiyo maana, kile kidogo walichojinyima wanakiweka mikononi mwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kiweze kuwafariji wale wanaohitaji zaidi. Wanamshukuru kwa unyenyekevu na ujasiri mkubwa katika kulihudimia Kanisa la Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.