2013-02-16 08:45:52

Hekima na busara, kamwe havizeeki! Papa Benedikto XVI amedhihirisha hilo!


Shimon Peres Rais wa Israel anasema, amesikitishwa sana na uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kung'atuka madarakani. Huu ni uamuzi wa busara, hekima, ujasiri na moyo mkuu, kielelezo na mfano wa kuigwa katika ushupavu wake.

Papa Benedikto wa kumi na sita, amechangia kwa kiasi kikubwa kutokana na mawazo yake yaliyosheheni hekima na busara. Kama binadamu, mwili unaweza kuzeeka na kudhoofu, lakini hekima na busara kamwe haviwezi kuzeeka. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea amani, utu na heshima ya binadamu; kielelezo cha imani katika utendaji; mtu mwenye uwezo wa kusoma alama za nyakati na kutoa maamuzi magumu; tofauti za kibinadamu zisiwe ni chanzo cha kujenga chuki na uhasama.

Rais Peres anaendelea kueleza kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uhusiano wa kidini kati ya Wayahudi na Wakristo kwani kuna undugu kati yao. Mwenyezi Mungu bado anaendelea kufanya hija na Waisraeli.

Papa Benedikto wa kumi na sita, ametembelea Israeli na Hekalu kuu la Roma, kama kielelezo cha urafiki na mshikamano wa kweli. Alipokuwa Israeli, Rais Peres anasema, alibahatika kuwa karibu zaidi na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, akasali kwa ajili ya kuombea amani Mashariki ya Kati, kama wanavyofanya hata viongozi wengine.

Pengine ni makosa kufikiri kwamba, Papa ni kiongozi wa Vatican kama walivyo wengine! Baba Mtakatifu ni kiongozi wa maisha ya kiroho, mwenye uwezo na busara ya ajabu kabisa! Rais Peres anasema, kwake Papa ni Rafiki na kweli anamtakia kila la kheri katika ukurasa mpya wa maisha yake, anasema, ataendelea kuwasiliana naye. Yerusalemu itasali kwa ajili ya kumwombea ili aweze kupata nguvu ya kimwili ili kuendelea kushirikisha hekima na ufahamu wake kwa watu na dini mbali mbali, kwa hakika, atakumbukwa kwa mambo mengi aliyotenda!







All the contents on this site are copyrighted ©.