Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima
Mpendwa mwana wa Mungu tayari tuko kipindi cha kwaresima, kipindi cha mfungo mtakatifu.
Tunatafakari pamoja masomo Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha kwaresima ya mwaka C
wa Kanisa. Neno la Mungu latuwekea mbele yetu ushiriki wa Mungu katika matatizo ya
mwanadamu.
Tunamwona
Bwana anayejaribiwa na shetani lakini pia ambaye anashinda vishawishi hivyo kwa nguvu
ya Mungu. Ushiriki wake katika mateso ya mwanadamu ni namna pia ya kuonesha uaminifu
wake katika ahadi alizozitoa kwa taifa la Israeli. Sote twatambua, katika Agano la
Kale aliwahaidi Wana wa Israeli kwamba atawapatia nchi ya ahadi, na hivi katika somo
la kwanza tunaona anakamilisha hilo na Waisraeli wanahaidi kushika Agano kati yao
na Mungu. Namna ya kushika agano lao na Mungu, watatoa malimbuko ya nchi kama shukrani
kwa Mungu wao. Watawafundisha watoto wao sala ya agano lao daima katika maisha yao.
Bwana
wetu Yesu Kristo anajaribiwa jangwani na anashinda, hili ni fundisho kwa wale wote
wanaomfuata, yakwamba katika maisha yao ya Kikristu wasitarajie maisha lelemama bali
maisha dhabiti ambayo mmoja anapaswa kuwa imara, akichota uimara huo katika Roho Mtakatifu
na akimfuasa Bwana aliyejaribiwa na hatimaye kushinda. Bwana anapokuwa jangwani anafunga
siku arobaini na hivi kwa njia hiyo anawasiliana na Baba yake, anajitenga na ulimwengu,
anakusanya nguvu kwa ajili ya mapambano dhidi ya mwovu na kwa ajili ya utume wake
wa kumwokoa mwanadamu. Mwaliko kwetu nasi, ni maisha ya jangwani yaani maisha ya sala,
maisha ya kufunga na kujitakatifuza kwa njia ya sakramenti ya kitubio na Ekaristi
Takatifu.
Mwovu shetani kadiri ya Injili anamtembeza Bwana na kumwonesha mali
zote za dunia na fahari zote, akitaka kusema kuwa mambo ya kidunia yaweza kuwa ya
maana kushinda yaliyo ya mbinguni, lakini Bwana akijua hila za mwovu huyu akimtii
Baba yake wa mbinguni anajibu akisema imeandikwa usimjaribu Bwana Mungu wako, bali
ukamsujudie Bwana Mungu wako na umwabudu yeye peke yake. Bwana anatuonesha jinsi ambavyo
mwanadamu anaweka nguvu katika kutazama mambo ya dunia hii badala ya mambo ya kimungu.
Kumbe sasa tunaalikwa kutazama zaidi mambo ya mbinguni kwa njia yake.
Mwovu
shetani anajaribu kumwambia Bwana kuwa Mungu atakuagizia malaika waje kukulinda, huu
ni mfano wa mbinu mbalimbali ambazo shetani hutumia kumwangusha mwanadamu. Habari
juu ya malaika yataka kujenga mazingira ili Bwana aingie katika kiburi, lakini Bwana
akijua kuwa kwa njia ya unyenyekevu ataweza kushinda anatupilia mbali hoja hiyo. Vivyohivyo
inapaswa kuwa kwa mwanadamu, kupembua upumbavu wa mwovu shetani mapema na kuutupilia
mbali. Hili huwezi kulitambua bila nguvu ya sala, bila kukaa jangwani ukifunga na
kumwimbia Mungu tenzi za rohoni.
Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anasema
kwa kuwa tumekombolewa tayari, linalobaki ni kumkiri Yesu Kristu kwa kinywa chako,
na kwa namna hiyo hutaweza kubabaika katika maisha na safari yako ya kikristu ukielekea
mbinguni. Kumkiri Bwana si kuinuka na kutangaza majukwaani bali kufuata mfano wa Bwana
katika kufunga na kusali ili kujipatia fadhila mbalimbali ambazo zatujaza neema kwa
ajili ya wokovu wetu na wengine.
Kumkiri Bwana ni kutimiza mapenzi yake yaani
kwenda mpaka msalabani kama yeye alivyofanya. Ni kuishi upendo mkamilifu yaani unaoshirikisha
furaha itokayo katika fumbo la msalaba. Kumkiri Bwana ni kushika Torati kama ambavyo
wana wa Israeli walivyohaidi kufanya walipotoka utumwani Misri na hata wakaweza kutoa
malimbuko ya kazi ya mikono yao. Malimbuko haya waliyoyatoa kwa Bwana yalitumiwa na
wajane, yatima na Walawi. Hili latuonesha upendo wao kwa Mungu na viumbe vyake. Kumbe
kumkiri Bwana ni pia kumtolea shukrani toka kazi ya mikono na akili yako katika unyenyekevu.
Mpendwa
mwana wa Mungu, kipindi cha kwaresima ni kipindi cha kupanda mbegu na kufanya palizi
ili baadaye tuweze kupata mavuno mazuri. Kumbe jiweke katika mwelekeo huo ili usije
baadaye ukakosa mazao na kuingia kwenye baa la njaa, yaani kukaukiwa neema za Mungu.
Nikutakie mpando mwema na palizi angalifu ili tukutane tukiwa wa furaha mwishoni mwa
kwaresima yetu, ndiyo uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa
kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.