2013-02-15 15:03:18

Nigeria kufanya kongamano la kitaifa kuhusu haki, amani na upatanisho mintarafu "Dhamana ya Afrika"


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kuanzia tarehe 11 hadi 16 Machi 2013, litafanya Kongamano la Kitaifa kujadili: haki, amani na upatanisho mintarafu Waraka wa kichungaji uliotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Africae Munus, Dhamana ya Afrika, uliotolewa mwezi Novemba 2011 nchini Benin. Ni waraka ambao kwa sasa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Lengo la Kongamano hili wanasema Maaskofu wa Nigeria ni kuwajengea waamini na wananchi uwezo wa kushughulikia kinzani na migogoro inayofumbatwa katika kinzani za kiiimani na kikabila; mambo ambayo yanakuja kwa kasi ya ajabu Barani Afrika, hata baada ya kusherehekea Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa bendera. Wadau na wawezeshaji kutoka ndani na nje ya Nigeria, watashirikisha uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika kushughulikia kinzani na migogoro ya kidini na kikabila sehemu mbali mbali za dunia.

Pamoja na mada nyingine zilizokwishabainishwa tayari, Maaskofu watajikita zaidi katika kuangalia Madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo na Uelewa makini juu ya dhana ya Wafiadini mintarafu hali ya mazingira ya Nigeria; yaliyomo na fursa zilizopo. Wajumbe wataangalia uelewa wa Yesu kwa waamini wa dini nyingine nchini Nigeria pamoja na Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Dini na Vurugu; Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee nchini Nigeria na waamini wa dini ya Kiislam.

Washiriki watapata fursa ya kusikiliza Injili ya Amani kadiri ya Mafundisho ya Yesu sanjari na misingi ya ujenzi wa amani katika Jamii yenye waamini wa dini mbali mbali. Majadiliano na tafakari zote hizi, zinalenga kwa namna ya pekee kuwajengea uwezo waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba, Kongamano hili linaweza kuhudhuriwa na watu wote wanaopenda kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano, haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, dini ni kielelezo cha imani na kamwe isitumiwe na wajanja wachache ili kuvuruga amani na utulivu kwa ajili ya mafao yao binafsi, kama inavyojionesha kwa nchi nyingi za Kiafrika, kwani imegunduliwa kwamba, chokochoko na vurugu za kidini sasa ni mtaji kwa baadhi ya watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka wanaotaka kupeta kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.








All the contents on this site are copyrighted ©.