2013-02-15 07:33:53

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama unavyochambuliwa na Papa Benedikto XVI


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi, tarehe 14 Februari 2013 amewaacha Makleri wa Jimbo kuu la Roma wakiwa wameshika tama kutokana na umahiri wake wa kuchambua yale yaliyojiri wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akihubiri kwa macho makavu kabisa. Amekazia umuhimu wa Jimbo la Roma kuhamasisha miito mitakatifu ya maisha ya kipadre na kitawa, kwa kuonesha ile karama ya kimataifa ambayo kimsingi ni utambulisho wa Jimbo la Roma.

Anawashukuru na kuwapongeza kwa kusali Kanuni ya Imani kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani. Makleri wanapaswa kuungama na kumtolea Kristo ushuhuda wa maisha yao amini. Anawashukuru kwa sala na majitoleo yao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema, kama Jaalim wa Chuo Kikuu cha Bonn, Ujerumani, alikuwa ameshirikishwa na viongozi wa Kanisa kuchangia hoja kuhusu Mtazamo wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa vatican katika mawazo ya Ulimwengu mamboleo. Papa Yohane wa ishirini na tatu, akatambua na kuthamini mchango wa mawazo yake, kiasi kwamba, akamteua kuwa ni kati ya wataalam walioshiriki katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Akamteua kuwa ni mshauri wake binafsi.

Hii ilikuwa ni Pentekoste Mpya kwa Kanisa Katoliki, kwa kutaka kusoma alama za nyakati, kusahihisha mapumgufu yake, ili hatimaye, liweze kushirikiana na wadau mbali mbali ili kumletea mwanadamu maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakatambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbali mbali na hatimaye, kuvipigia kura.

Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maaskofu na Makardinali wengi walishiriki kikamilifu katika kupembua na kujadili hali ya maisha na utume wa Kanisa. Kwanza kabisa anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Mababa wa Mtaguso walitaka kufanya marekebisho makubwa kwenye Liturujia; Kanisa, Neno la Mungu, Ufunuo na Majadiliano ya Kiekumene. Baadhi ya Mababa wa Mtaguso walitaka Kanisa lijadili kuhusu uhusiano kati ya Serikali na Kanisa.

Mabadiliko ya Liturujia ya Kanisa yalipania kuhakikisha kwamba, waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kwa kutumia lugha na maneno ambayo yaligusa undani wa mioyo ya watu, daima wakiwa na utambuzi makini wa Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Mababa walitamani kuona kwamba, majadiliano yanayofanyika ndani ya Kanisa yanawagusa watu wote.

Huu ukawa ni mwanzo wa dhana ya ushiriki mkamilifu katika matendo na alama mbali mbali za Kiliturujia ndani ya Kanisa, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza, kwani ndiye anayepaswa kuheshimiwa, kuabudiwa na kutukuzwa na watu. Maadhimisho ya Siku ya Bwana, yakapewa msukumo wa pekee, kama siku ya Mungu, Siku ya Kristo, Siku ya Mwanadamu na Siku ya kutafakari mambo ya nyakati. Watu wakahamasishwa kusali na kulisikiliza Neno la Mungu katika lugha zao asilia.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wakakazia kuhusu majiundo makini ya Makleri kwa kuwataka kuyafahamu Maandiko Matakatifu, yaani Agano Jipya na Agano la Kale kwa ufasaha mkubwa, ili waweze kuwafafanuliwa waamini wao, kama sehemu ya chakula cha kiroho, ili hatimaye, waweze kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Kristo pamoja na Kanisa lake. Mababa wa Mtaguso wakatambua kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo; lenye asili mbili: Umungu kwani limeanzishwa na Kristo; Pili lina asili ya Kibinadamu kwani Kristo amewakabidhi binadamu kuliongoza; hawa ni watu wenye karama na mapungufu yao.

Kanisa likajitambua kuwa ni Jumuiya ya Waamini wanaomwamini Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hili ni Kanisa ambalo Kristo amelikabidhi chini ya uongozi wa Mtakatifu Petro na utume huu unaendelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia ni waandamizi katika utekelezaji wa dhamana na utume wa Mama Kanisa ulimwenguni. Wote hawa wanaunganishwa na kuwa ni kitu kimoja kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kila Askofu akiwa na haki na wajibu wake mbele ya Kanisa la Kristo.

Makleri pamoja na Waamini Walei wanaunda Taifa la Mungu, kama mwendelezo wa historia ya ukombozi iliyoanzishwa na Mungu mwenyewe. Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatican wakabainisha chemchemi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Taifa la Mungu; Fumbo la Mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Umoja katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ukatiliwa mkazo kama chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Umoja huu unapaswa kujionesha kwanza kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu, kama lilivyo Fumbo la Utatu Mtakatifu: Umoja katika Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Umoja na Maaskofu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Kuhusu Neno la Mungu na Ufunuo; Mababa walibainisha kwamba, Neno la Mungu ni sehemu ya urithi wa Kanisa na lina dhamana ya kujenga na kuimarisha Kanisa lenyewe, kumbe kuna umuhimu wa kuheshimu na kutunza Mapokeo ya Kanisa. Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha ya mtu anapokuwa katika hija ya kuelekea katika Fumbo la Kifo. Maandiko Matakatifu ni urithi wa Kanisa, kielelezo makini cha imani na kwamba, Kanisa linadhamana ya kutoa tafsiri sahihi ya Neno la Mungu. Hapa anasema Baba Mtakatifu, ile kazi iliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican bado inapaswa kufanyiwa kazi zaidi.

Majadiliano ya kiekumene anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yalilenga kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa wafuasi wa Kristo; hii ni hija ambayo Kanisa bado linaendelea kuifanya kwa matumaini kwamba, kwa mapenzi ya Kristo mwenyewe, iko siku Wakristo wataweza kuwa wamoja chini ya Mchungaji mmoja. Hapa Wakristo wanawajibika kusimama kidete kulinda na kutetea kanuni maadili, uhuru wa kidini pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine, ili kudumisha amani, utulivu na maelewano. Mababa wa Mtaguso wakatambua na kuthamini umuhimu wa majadiliano ya Kidini pamoja na huduma kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu.

Kanisa bado lina changamotishwa kuendeleza majadiliano ya kina na waamini wa dini ya Kiislam, hasa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Majadiliano ambayo yanaonesha utofauti wa imani, umoja na mshikamano kwa kutambua kwamba, Mungu ni mmoja; ni Neno aliyefanyika Mwili. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, uhuru wa kidini, majadiliano ya kidini na maendeleo endelevu ni mambo ambayo yalipembuliwa kwa kina na mapana, umuhimu wake umeanza kuonekana baadaye kabisa! Waamini wa dini na Madhehebu mbali mbali wanachangamotishwa kutokana na imani yao, kuchuchumilia misingi ya haki, amani na utulivu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitambua umuhimu wa njia za mawasiliano ya Jamii kuwa ni mchakato wa imani inayotaka kukumbatia akili ya mwanadamu kwa kusoma alama za nyakati. Njia za mawasiliano ya Jamii zilionekana kana kwamba, ni mapambano yaliyopania kujipatia madaraka na kuwagawanya Watu wa Mungu: yaani Makleri, Watawa na Waamini Walei. Papa akapewa madaraka ya juu kabisa, wakafuatia Maaskofu mahalia na hatimaye kwa waamini walei. Hapa kukazuka hali ya kutoelewana ndani ya Kanisa.

Waamini walei wakajikuta wanajitwalia madaraka ambayo si yao! Hapa mawazo ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yakapakwa tope na hivyo kushindwa kufahamika barabara! Mageuzi ya Kiliturujia yakakosa dira na mwelekeo, Maandiko Matakatifu, kikawa ni Kitabu cha Historia. Matokeo yake anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Kanisa likajikuta likiandamwa na matukio ya ajabu kabisa: Seminari na nyumba za kitawa zikafungwa; Maadhimisho ya Liturujia yakakosa heshima na utakatifu wake unaopania kumtukuza Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ukajikuta umesimama njia panda!

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, liwe ni tukio linaloonesha ile nguvu ya kiroho inayopania kuleta mabadiliko ya kweli na ya dhati ndani ya Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, iko siku Kristo atashinda!

Mazungumzo ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI yamehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.