2013-02-15 10:33:52

Kamwe dini zisiwe ni chanzo cha choko choko na vurugu za kidini Barani Afrika! Hizi ni njama za wajanja wachache kutaka kutajirika!


Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria anasema, kuna haja kwa wananchi Barani Afrika kuhakikisha kwamba, wanaondokana na kasumba za kikoloni zilizotumika kuwagawa watu kwa misingi ya kidini ili kuwatawala kwa urahisi.

Majadiliano ya kidini, amani na utulivu ni jambo muhimu sana katika ulimwengu wa utandawazi na kamwe ukabila na dini situmiwe na wajanja wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi kwa kusababisha maafa makubwa katika Jamii kama inavyojionesha nchini Nigeria. Katika miaka ya hivi karibuni kumezuka wimbi kubwa la machafuko ya kidini, hali ambayo imechafua kwa kiasi kikubwa upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa uliokuwepo kwa miaka kadhaa iliyopita. Baadhi ya viongozi wa kidini wamekuwa wakiwatumia vijana kuanzisha vurugu na matokeo yake ni maafa makubwa kwa Jamii na ni kikwazo kikuu cha maendeleo na ustawi wa Kijamii.

Ili kuondokana na dhana potofu kuhusu dini, kuna haja kwa viongozi wa kidini kutoa mafundisho ya kina kuhusu dini zao, daima wakitetea haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kuna baadhi ya waamini wanadhani kwamba, kuna dini ambazo zimebahatika kutoa miujiza na kwamba, wanakwenda huko kwa imani kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu atawapatia muujiza wao na hivyo kuwa na hali nzuri kiuchumi, kijamii pamoja na kuwaondolea magonjwa au balaa zinazowaandama katika maisha.

Askofu mkuu Kaigama anasema, uwezo mdogo wa kufikiri kwa baadhi ya watu, wamejikuta wakitumbukizwa katika imani za kishirikina, kwa kudhani kwamba, viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vina fumbata bahati na matokeo yake ni wimbi la mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kama ilivyo pia kwa mauaji ya vikongewe sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Jamii iwekeze katika elimu, afya na maendeleo endelevu, watu waondokane na imani, mila, desturi na tamaduni zilizopitwa na wakati. Wananchi wajifunze kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na bidii, wajitahidi kupata riziki kwa kufanya kazi halali na kwamba, hakuna njia ya mkato ili kupata mafanikio.

Tofauti za kidini na kikabila ni sehemu ya maisha ya watu, kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthaminiana, kamwe dini zisiwe ni chanzo cha choko choko na vurugu katika Jamii, bali iwe ni nguzo inayojenga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Askofu mkuu Kaigama ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anatoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Colon, nchini Ujerumani.







All the contents on this site are copyrighted ©.