Baba Mtakatifu Benedikto XVI akutana na Makleri wa Jimbo kuu la Roma
Kwa niaba ya Makleri wote wa Jimbo kuu la Roma, Kardinali Agostino Vallini, Makamu
Askofu Jimbo kuu la Roma, Alhamisi, tarehe 14 Februari, 2013, alimshukuru Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita kwa kukubali kuitikia wito wa kuweza kukutana na kuzungumza
na Makleri wake, ili kuwamegea utajiri mkubwa ambao watautunza kama hazina kubwa wanapotekeleza
majukumu yao kwa Familia ya Mungu, Jimboni Roma.
Anasema, mioyo yao imegubikwa
na hamu ya kutaka kusikiliza kwa makini wosia kutoka kwa Mchungaji mkuu wa Kanisa
anapokaribia kung’atuka kutoka madarakani, kama walivyofanya wazee walipokuwa wanamsikiliza
Mtume Paulo. Alipokuwa anawaaga, akiwakumbusha kwamba, kati yao, amejitahidi kumtumikia
Kristo kwa moyo na unyenyekevu mkubwa, kwa machozi na majaribu mengi, lakini bila
ya kukata tamaa. Amewahubiria na kuwashuhudia kuhusu umuhimu wa kumwongokea Mungu
pamoja na kuwa na imani thabiti kwa Kristo. Hata wao wana mioyo mizito iliyosheheni
mambo mengi, wanakubali na kuthamini maamuzi yake.
Kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, amewafundisha kuwa wafuasi amini wa Kristo na wachungaji bora; wakijitahidi
kutolea ushuhuda wa maisha ya kujitoa kimaso maso kwa Kristo na Kanisa lake bila ya
kujibakiza hata chembe kidogo! Wawe na imani inayoonesha ujasiri; unyenyekevu katika
huduma, daima wakichuchumilia ukweli na hamu ya kutaka kuhubiri Injili ya Kristo;
wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; hususan maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mwaka wa Imani ambao Mama Kanisa anaendelea kuuadhimisha
ni changamoto kubwa ya kufanya toba na kuchuchumilia utakatifu wa maisha kama kielelezo
makini cha huduma kwa watu wa Mungu.
Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni ufunguo muhimu sana katika kuyafahamu maisha na
utume wa Kanisa, wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni mwaliko
wa kuona mwendelezo wa Mapokeo ya Kanisa, kujibidisha kuzifahamu hati na nyaraka mbali
mbali za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kuwashirikisha wengine, kama nyezo
muhimu sana ya kuleta mabadiliko ndani ya Kanisa.
Ndiyo maana, Makleri wa
Roma wamemwomba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyeshiriki katika Maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuwashirikisha yale yaliyojiri wakati wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican, miaka 50 iliyopita! Makleri wa Jimbo kuu la Roma wanasema,
wataendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa njia ya sala
na sadaka zao.