Ratiba ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuelekea kwenye uchaguzi wa Papa Mpya
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika katekesi yake, Jumatano tarehe 13
Februari 2013 amebainisha mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutamka
wazi wazi kwamba, ameamua kung'atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru kamili
kwa ajili ya mafao ya Kanisa.
Anatambua kwamba, Kanisa ni mali ya Kristo,
ataliongoza na kulisimamia kwa kuliwezesha kupata tena mchungaji mkuu. Huu ni uamuzi
ambao unafumbata tafakari ya kina na imani thabiti, kwamba, Kristo anaendelea kuliongoza
Kanisa lake kwa njia ya neema na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ni mwaliko kwa waamini
na watu wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya Kanisa na kwa Papa anayekuja.
Ni
ufafanuzi wa Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican, wakati huu dunia inapoendelea
kujiuliza na kutafakari uamuzi wa hekima na busara uliochukuliwa na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, kwa kuamua kung'atuka kutoka madarakani. Anatambua kwamba,
wakati wote huu, ameendelea kusindikizwa kwa sala za Kanisa na waamini kutoka pande
mbali mbali za dunia. Anakazia toba na wongofu wa ndani kuwa ni mambo yanayopaswa
kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya Mkristo.
Toba anasema Baba Mtakatifu
si hali ya mtu kujitafuta mwenyewe, bali ni ushuhuda unaojionesha katika ukweli, imani
na mapendo thabiti katika uhalisia wa maisha ya mwamini; mambo yanayopaswa kupewa
msukumo wa pekee kabisa kwa kuyamwilisha. Baba Mtakatifu anayasema haya yote kwa kuwa
wakati wote wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejitahidi kuyamwilisha
katika uhalisia wa maisha.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi,
jioni anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Seneti Mario Monti, aliyekuwa Waziri mkuu
wa Italia. Rais Giorgio Napolitano wa Italia anatarajiwa kukutana na hatimaye kuagana
na Baba Mtakatifu tarehe 23 Februari 2013 baada ya Baba Mtakatifu kutoka katika Mafungo
yake ya kiroho na Rais Napolitano kurejea kutoka Marekani.
Baba Mtakatifu
atakuwa pia na mazungumzo ya faragha na baadhi ya Makardinali Jumatatu, tarehe 25
Februari 2013. Kwa wakati huu, hija za kitume zilizokuwa zimepangwa kwa Maaskofu mbali
mbali zimefutwa. Tarehe 27 Februari 2013, Baba Mtakatifu atahitimisha Katekesi zake
kwa siku ya Jumatano, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini
kutoka sehemu mbali mbali kama kielelezo cha shukrani na ukarimu kwa Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita.
Tarehe 28 Februari 2013, Makardinali watapata fursa
ya kuweza kuagana rasmi na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Hii itakuwa ni
nafasi kwa Kardinali mmoja mmoja kuzungumza na Papa kwa faragha, ikiwa kama anataka.
Saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atapanda
Elikopta kuelekea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Saa 2:00 Usiku. Kiti cha Khalifa
wa Mtakatifu Petro, kitakuwa wazi na hapo mchakato wa kuanza kumpata Papa mwingine
utaanza kushika kasi.
Katika kipindi hiki chote, Kardinali Caerlengo Tarcisio
Bertone atasimamia na kuratibu shughuli za Vatican. Wakati wote huu, Makardinali wataendelea
kufanya vikao mbali mbali kama njia ya kufahamiana, kubadilishana mawazo, kupembua
na kubainisha vipaumbele na changamoto zinazolikabili Kanisa kwa sasa na kwa siku
za usoni sanjari na mwelekeo wa mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya. Tarehe rasmi ya
uchaguzi wa Papa itapangwa na Makardinali wenyewe, ambayo inapaswa kuwa ni kati ya
tarehe 15 hadi tarehe 19 Machi 2013.
Baada ya kuchaguliwa kwa Papa Mpya, Makardinali
wataendelea na utaratibu uliowekwa na kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, hatahusika kwa jambo lolote kwa wakati huu, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuingilia
mchakato wa uchaguzi wa Papa. Anaweza kuandika ujumbe wa kitaalimungu kwa ajili ya
watu wa Mungu, akipenda. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukujuvya
habari mbali mbali, kadiri zinavyotolewa na Vatican. Unaweza pia kuwashirikisha wenzako
kuhusu mtandao huu ili kuweza kujipatia ufahamu mkubwa zaidi kuhusu maisha na utume
wa Kanisa.