2013-02-14 10:01:33

Ni matumaini ya Benedikto XVI kwamba, IFAD itaendeleza mikakati ya maboresho ya wakulima vijijini, kama kielelezo cha mshikamano na udugu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 13 Februari 2013 amemwandikia ujumbe Bwana Kanayo F. Nwanze, Rais wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD wakati huu wanapoendelea na mkutano wao wa 36. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele kutumia rasilimali zake kwa ajili ya wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, mikakati ya IFAD kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini katika mchakato wa maboresho ya maisha ni jambo ambalo Vatican inalipongeza sana.

Hizi ni juhudi zinazopaswa kuongozwa na kanuni maadili katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na katika harakati za ushirikiano wa kimataifa, katika mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa pamoja na kuendeleza juhudi za kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, sanjari na kutoa fursa za ajira na ushirikishwaji katika utoaji wa maamuzi, kwa kuwashirikisha wakulima wadogo wadogo vijijini katika maamuzi yanayowagusa.

Baba Mtakatifu inaipongeza IFAD kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa mradi wa mikopo vijijini, ili kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo wa kiuchumi pamoja na kushiriki katika kutoa maamuzi. Pili ni matumizi bora ya maliasili kwa ajili ya mafao ya Familia ya binadamu.

Utambulisho wa wakulima hawa ni jambo linalopaswa kupewa msukumo wa pekee, ili kuwasaidia kutunza tamaduni zao njema pamoja na kujenga mshikamano na nchi wahisani katika sekta ya kilimo. Mkakati huu unatambua kwamba, sekta ya kilimo ni uti wa mgongo na kikolezo cha maendeleo ya Jamii nyingi duniani, jambo linalohitaji kuongozwa na kanuni auni, makini kwa kutambua na kutekeleza mahitaji ya Jamii husika.

Katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, msisitizo unawekwa kwa mtu, kazi na ardhi, ili kuweza kubainisha sera na mikakati ya kisiasa na kiuchumi itakayowaletea watu maendeleo endelevu; IFAD inaonekana kutekeleza kwa makini mwelekeo huu pamoja na kuendelea kuhimiza vyama vya ushirika miongoni mwa wakulima wadogo wadogo, kama njia ya kuboresha hali ya maisha ya wakulima vijijini.

Mwakani, Jumuiya ya Kimataifa itaadhimisha Mwaka wa Familia Vijijini, kwa kuhimiza uelewa makini katika sekta ya kilimo, kama kikolezo cha maendeleo na mapambano dhidi ya umaskini kutoka katika Familia. Mikakati yote hii inapaswa kuzingatia sheria maadili, kwa kutoa mafunzo, pembejeo pamoja na kuhimiza uanzishwaji wa vyama vya ushirika vitakavyokoleza shughuli za uzalishaji katika sekta ya kilimo na hivyo kuboresha pia maisha ya wananchi wengi vijijini.

Ni mwanzo wa mapinduzi ya kilimo kwa nchi changa zaidi duniani, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashikamana kwa dhati katika utekelezaji wa mikakati kwa ajili ya wakulima wanaoishi vijijini. Rasilimali iliyopo kwa sasa anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa ni kidogo sana, kutokana na baadhi ya wafadhili kupunguza misaada na mchango wao kama sehemu ya kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Kuna haja ya kujenga mshikamano na kujali mahitaji ya wengine.

IFAD ni kati ya Taasisi za Kimataifa ambazo zimefanikiwa kuunganisha haki mpya za kimataifa na mshikamano wa dhati. Upendo wa dhati unaweza kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia maskini kwa kujenga ari ya udugu na ukarimu. Hapa anasema Baba Mtakatifu ni kutambua usawa ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia watu wote.

Ni matumaini yake kwamba, IFAD itaendelea kutekeleza mikakati ya maboresho ya maisha ya wakulima wengi vijijini kama kielelezo cha mshikamano wa dhati, ili kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi si tu kwa njia ya maendeleo ya teknolojia na weledi, bali pia kwa kuwajengea watu matumaini makubwa zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.