2013-02-14 08:02:15

Familia ya Mungu inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa unyenyekevu na ujasiri wake!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano ya Majivu, tarehe 13 Februari, 2013, kwa niaba ya Familia ya Mungu, alimshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa uamuzi wake wa ujasiri na hekima, miaka minane ya uongozi wake, amekuwa ni dirisha wazi kwa Kanisa na Ulimwengu, kwa kuonesha miali ya ukweli na upendo wa Mungu; kwa kutoa joto katika hija ya maisha ya Kanisa hata pale giza nene lilipoonekana kana kwamba limetanda angani na hivyo kutishia amani!

Baba Mtakatifu ameonesha upendo mkubwa kwa Mungu na Kanisa, kwa kuonesha usafi wa roho, imani thabiti, unyenyekevu na ujasiri; mambo yaliyoacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Haya ni matokeo ya mtu aliyeshibana kwa kiasi kikubwa na Mwenyezi Mungu, anayefanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, daima akijitahidi kukwea Mlimani ili kuweza kukutana na Muumba wake katika faragha, ili hatimaye, kushuka na kuwasaidia wajenzi wa dunia.

Daima watakumbuka maneno yake kwa Jumuiya ya Seminari kuu ya Roma kwamba, yale yajayo yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Kanisa litaendelea kukua na kukomaa. Huduma katika ujenzi wa Kanisa ni kazi inayofanywa na Mwenyezi Mungu mwenyewe, binadamu ni kama chombo kisichokuwa na faida.

Kardinali Bertone, anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kufanya uamuzi huu mgumu na wa busara, mfano na kielelezo makini kwanza kabisa kwa viongozi wa Kanisa na kwa Familia ya Mungu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu ni kielelezo cha shukrani mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kanisa linamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa hija ya maisha na utume wake katika kipindi cha miaka minane, kwa hakika amekuwa ni mwanga angavu na mfano wa mfanyakazi mnyenyekevu katika shamba la Bwana, aliyetambua daima kwamba, anayo dhamana ya kumpeleka Mungu kwa watu na kuwapeleka watu kwa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.