2013-02-14 07:53:41

Benedikto XVI atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, limemwandikia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, barua ya shukrani kutokana na uaminifu, ujasiri na majitoleo makubwa aliyoyaonesha wakati wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; dhamana ambayo ilisheheni utajiri mkubwa wa mafundisho pamoja na huduma mbali mbali alizozitoa kwa ajili ya Watu wa Mungu Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu ameonesha ukomavu wa imani kwa kumwaminia na kumwonesha Yesu Kristo mapendo ya hali ya juu kwa njia ya Kanisa lake. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, wakati huu linapenda kumwonesha Baba Mtakatifu upendo na uwepo wao wa karibu katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha na utume wake.

Wanapenda kumhakikishia kwamba, wataendelea kulihudumia Kanisa kwa ari na imani ambayo Baba Mtakatifu mwenyewe ameionesha na kuishuhudia. Barua hii imetiwa mkwaju na Kardinali Peter Erdo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Bara la Ulaya kwa niaba ya viongozi wakuu wa Shirikisho hili.

Wakati huo huo, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene aliouonesha wakati wa uongozi wake, kama: Mwanataalilimungu mahiri, Mtaalam wa Mababa wa Kanisa na mwenye upeo mkubwa kwa masuala mamboleo.

Anasema, amesikitishwa na taarifa ya kung’atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka madarakani na kwamba, anaacha chapa ya kudumu katika mchakato wa kudumisha majadiliano ya Kiekumene yaliyojikita katika ushuhuda wa maisha adili na historia ya Kanisa Katoliki. Miaka minane si haba!

Daima Baba Mtakatifu amekuwa akijikita katika kushughulikia masuala ya utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Waamini wa Kanisa la Kiorthodox wataendelea kukumbuka hija ya kichungaji aliyoifanya kwenye Kanisa lao wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.








All the contents on this site are copyrighted ©.