Matendo ya huruma yaongozwe na: imani na matumaini kama kielelezo cha mshikamano wa
dhati!
Shirikisho la Vyama vya Mtakatifu Vinsenti wa Paulo Kimataifa, lililoanzishwa yapata
miaka 180 iliyopita na kuwa na wanachama zaidi 780,000, wanaowahudumia maskini zaidi
ya millioni 30; linaongozwa na kanuni ya imani, matumaini na mapendo yanayobubujika
kutoka katika kweli za Kiinjili. Ni Shirikisho
linalopania kumhudumia mtu mzima katika mahitaji yake ya kiroho na kimwili. Hawa ni
watu walioathirika kutokana na umaskini, magonjwa na ujinga. Watu ambao wakati mwingine
wanajikuta wametumbukizwa katika umaskini kutokana na vita, migogoro, kinzani, majanga
asilia pamoja ubinafsi wa watu kama inavyojionesha katika athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Ni Shirikisho ambalo limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa kutoa huduma
katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu, ili kuweza kumletea mwanadamu ukombozi
kamili. Limekuwa likitoa msaada wa mikopo midogo midogo, ili kuwajengea wananchi uwezo
wa kupambana na maisha, ili hatimaye, waweze kujiletea maendeleo yao wenyewe! Kutokana
na ushiriki wake katika huduma ya upendo kwa watu wenye matatizo mbali mbali, Umoja
wa Mataifa mwaka 2012 ulilitambua Shirikisho la Vyama vya Mtakatifu Vinsenti wa Paulo
Kimataifa, kuwa ni kati ya Mwanachama wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Umoja wa
Mataifa katika huduma za Kijamii (ECOSOC). Huu ni ushuhuda uliotolewa na Dr. Michael
Thio, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Mtakatifu Vinsenti wa Paulo, wakati wa kuwasilisha
ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka
2013. Ni Shirikisho la Kimataifa linalotekeleza utume na dhamana yake katika ulimwengu
kwa kuongozwa na Imani, Matumaini na Mapendo. Haya ni matunda ya ukimya yanayobubujika
katika Sala; ni kielelezo cha Sala katika Imani na matunda ya Imani katika upendo
unaopania kudumisha amani. Hii ni sehemu ya tafakari ya kina kutoka kwa Mama Theresa
wa Calcuta, moja ya Watoto wa Kanisa waliojitoa bila ya kujibakiza ili kuwamegea maskini,
wasiopendwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ule upendo wa dhati unaobubujika
kutoka katika Imani kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto kwa kila mwamini kumwilisha
Imani yake katika matendo, hasa wakati wa Kipindi cha Kwaresima, Kipindi cha toba
na wongofu wa ndani; mwaliko wa kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu pamoja na
kuboresha maisha ya kiroho kwa njia ya Sakramenti za Kanisa.