2013-02-13 06:56:57

Madhulumu ya Wakristo nchini Nigeria ni jambo la kusikitisha sana! Ni vitendo vya kigaidi, sheria ichukue mkondo wake!


Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja anasema kwamba, madhulumu ya Wakristo nchini Nigeria ni tukio ambalo limelishtukiza Kanisa bila hata maandalizi na hakuna mtu aliyekuwa anawaza kwamba, kuna siku jambo kama hili linaweza kutokea nchini Nigeria, lakini huu ndio ukweli wa mambo. Watu wana hofu ya usalama wa maisha na mali yao; wanaogopa kwenda Kanisani, kusafiri au kubeba mabegi mazito.

Inasikitisha kuona kwamba, watu wenye msimamo mikali ya imani kama kilivyo kikundi cha Boko Haram wanasababisha uvunjifu mkubwa wa haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Hawa ni wavunjaji wa sheria, wanapaswa kutiwa pingu na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kujibu mashtaka yatakayokuwa yanawakabili, kwani hii si imani ya kweli inayoungamwa na waamini wa dini ya Kiislam.

Ni watu ambao hawana sheria, dira wala mwongozo wa maisha, wanataka kuvuruga amani na upatanisho, kwani vitendo kama hivi wanawatendea pia waamini wa dini ya Kiislam, kumbe kwa maneno machache vitendo vinavyofanywa na Kikundi cha Boko Haram ni vya kigaidi, vinapaswa kudhibitiwa kwa nguvu zote. Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kwa amanina utulivu; wakiheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini. Lakini kuna makundi ya watu wanaotumiwa na watu kutoka nje kwa ajili ya mafao yao binafsi ili kuvuruga amani.

Takwimu kutoka katika Taasisi ya Uchumi na Amani nchini Nigeria zinaonesha kwamba, tangu vitendo vya kigaidi na kujitoa mhanga vianze kujitokeza na hatimaye kushamiri nchini Nigeria, kuna Wakristo 700 waliouwawa kikatili kunako mwaka 2012. Katika miaka ya nyuma, wakristo 437 waliuwawa pia nchini Nigeria. Matukio ya kigaidi ni vitendo vinavyoratibiwa na kundi kubwa kutokana ndani na nje ya nchi husika.

Kardinali Onaiyekan ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa kwenye ziara ya kichungaji nchini Canada. Nigeria ina idadi ya watu wapatao million 80, licha ya uhusiano kati ya Wakristo na Waislam kupata mtikisiko mkubwa, lakini bado watu wengi wana amini kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuishi kwa amani na utulivu, kila mtu akiheshimu na kuthamini dini ya jirani yake. Ni jukumu la Baraza Kuu la Waislam Nigeria kudhibiti vitendo hivi ambavyo ni hatari kwa usalama, maisha na ustawi wan chi.

Watu washinde kishawishi cha kutaka kupata utajiri wa haraka haraka kwa fedha haramu zinazopatikana kutokana na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Wananchi washirikiana kwa dhati kutafuta mafao ya wengi, hali wakisimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; uhuru wa kidini pamoja na utawala wa sheria.








All the contents on this site are copyrighted ©.