2013-02-13 07:18:36

Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima mjini Vatican


Kwaresima ya Mwaka 2013 inaongozwa na kauli mbiu “Nasi tumelifahamu pendo alilonalo Mungu, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake” Kwa maneno machache Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini kumwilisha Imani yao katika Mapendo. RealAudioMP3
Mama Kanisa anakianza Kipindi cha Kwaresima, kwa Jumatano ya Majivu, ambamo waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kufunga kama sehemu ya kufanya toba ili kujiandaa kikamilifu katika hija ya ukombozi inayowapatia fursa ya kulitafakari Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo.
Ni kipindi cha Siku arobaini kinachowakumbusha waamini: ile miaka 40 ya shida na taabu; pale Waisraeli walipokiona cha mtema kuni kutokana na ukaidi wao kabla ya kuruhusiwa kuingia kwenye nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali. Musa alitumia siku 40 kufunga kabla hajapewa jukumu la kuandika Torati ambazo ni Amri za Mungu, dira, mwongozo na utambulisho wa Waisraeli kama Taifa teule la Mungu.
Itakumbukwa kwamba, Yesu kabla ya kuanza maisha na utume wake hadharani alifunga kwa muda wa siku 40, akapambana na Ibilisi, na kutoka Jangwani akiwa mshindi. Wafuasi wa Yesu walijifungia ndani kwa siku 40 baada ya ufufuko wa Kristo, wakiogopa kipigo na mkong’oto kutoka kwa Wayahudi, hadi siku ile waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, wakatoka kifua mbele kutangaza kwa ari na nguvu mpya kwamba: Kristo aliteswa, akafa na kufufuka, changamoto endelevu hata katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Ni kipindi cha muafaka kabisa kwa ajili ya kuwaandaa Wakatekumeni kuingia katika Mlango wa Imani, mwaliko kwa waamini kujikumbusha tena ahadi zao za Ubatizo; nafasi na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao ya kila siku.
Kwaresima ni Kipindi cha kufunga, ili kumwezesha mwamini kujenga na kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu; Maisha ya Kisakramenti, lakini zaidi kwa kupokea Sakramenti ya Upatanisho inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu. Inamkumbusha kwamba, ni mdhambi anahitaji kutubu na kumwongokea Mungu kama sehemu ya hija ya maisha yake hapa duniani. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inawachangamotisha waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma.
Mwaka wa Imani, uwe ni kielelezo cha Imani tendaji; kwani Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2013 anabainisha kwamba, imani na upendo ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa. Kufunga kuna faida kubwa hata katika maisha adili kwani kunamsaidia mwamini kuratibu vilema vyake, kujikubali na kuanza kujisahihisha ili kuweza kuwa ni mtu mwema zaidi kwa kuondokana pia na dhambi za mazoea. Mfungo uwawezeshe waamini kujenga dhamiri safi, daima wakijitahidi kuchagua jema la kufuata na baya la kuachana nalo!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na wasaidizi wake wandamizi watakuwa na Mafungo ya Kiroho kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka. Mafungo haya yanaongozwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Wazo kuu litakaloongoza mafungo haya ya kiroho “Uso wa Mungu, uso wa mwanadamu katika Zaburi” Kauli mbiu hii kwa lugha ya Kilatini inasomeka “Ars Orandi, Ars Credenti” Atapembua kwa kina na mapana maana ya maneno: kupumua, kufikiri, kupambana na kupenda mintarafu Sala ya Mzaburi. Ni tafakari inayolenga kuwashirikisha walengwa lile Fumbo na Mwanga wa Mungu unaoangazia uso wa mwanadamu.
Baba Mtakatifu amemkabidhi Patriaki Bechara Boutros Rai kuandaa Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Coloseo, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya hija ya kichungaji, iliyofanywa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita nchini Lebanoni, ili kuwasilisha Matunda ya Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Mashariki ya Kati. Tafakari hii itakuwa na vituo kumi na vinne kama yalivyo Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itaendelea kukushirikisha yale yatakayojiri katika Kipindi cha Kwaresima, kutoka pande mbali mbali za dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.