2013-02-13 09:41:50

Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho katika Jangwa la maisha ya mwamini inayojikita katika: Sala, Kufunga, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya Huruma


Ee Bwana utujalie sisi waamini wako tuanze vita vya kiroho kwa mfungo mtakatifu. Nasi tulio tayari kupigana na pepo wabaya tujipatie nguvu kwa sababu ya kufunga. Kwa maneno haya, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ambaye yuko nchini India kwa ziara ya kichungaji, aliwaalika waamini kukianza kipindi cha Kwaresima, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo.

Kwaresima kiwe ni kipindi cha kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Ni fursa ya kufunga na kusali. Majivu yawakumbushe waamini kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena, iwe ni alama ya toba na hamu ya kutaka kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Kila mwamini ajiwekee malengo atakayoyafanyia kazi wakati wa hija ya Kipindi cha Kwaresima, lakini zaidi wakijikita katika upatanisho na msamaha. Waamini warudie tena ahadi zao za ubatizo, kwa kuifia dhambi na hivyo kuanza mchakato wa kuambatana na Yesu katika hija ya maisha ya kila siku.

Kipindi cha Kwaresima, waamini wajitahidi zaidi na zaidi: kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma. Matendo yote haya yanamwelekea Mungu na jirani. Wakristo kama anavyosema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wanapaswa kuwa ni kielelezo cha upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, kwani upendo wa Kristo unawawajibisha hata nao kupenda hivyo hivyo!

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa ya pekee kwa Familia ya Mungu kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya kina. Mapadre wajitahidi kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu katika mahubiri yao ili kuzima kiu na njaa ya Neno la Mungu kati ya watu.

Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa yawawezeshe waamini kukutana na Yesu Kristo. Watawa wawe waaminifu kwa karama za Mashirika yao ambazo ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa; daima wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.