Jifunzeni kukubali, kuthamini na kupokea tofauti za kijamii, kisiasa, kidini na kikabila,
ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu!
Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya katika uzinduzi wa Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2013 amefafanua kwamba,
Baraza la Maaskofu litafuatilia kwa ukaribu mchakato wote wa uchaguzi lakini halitajihusisha
na Kampeni kwa ajili ya wagombea mbali mbali wanaowaminia nafasi ya uongozi nchini
Kenya.
Wananchi wa Kenya bado wanayo kumbu kumbu hai ya madhara na maafa makubwa
yaliyojitokeza mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Kenya
kunako mwaka 2007/2008. Wananchi wa Kenya wanataka kuona umoja wa kitaifa unaosimikwa
katika misingi ya amani, kwani vurugu na machafuko ya kisiasa yatapelekea maafa kwa
watu na mali zao.
Viongozi wanaowania madaraka wanapaswa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa mafao ya wengi, haki, amani na utulivu na kwamba, uchaguzi mkuu isiwe
tena ni chanzo cha kuwagawa wananchi wa Kenya. Wananchi wajifunze: kukubali, kuthamini
na kupokea tofauti zao za kijamii, kisiasa, kidini na kikabila.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Kenya katika kipindi cha Majuma manne, litaangalia kwa kina na mapana:
Juma la kwanza wataangalia kuhusu usalama na wajibu wa kila mwananchi; Juma la pili:
Uchaguzi mkuu; Juma la tatu: utawala wa Serikali za mitaa. Juma la nne Upatanisho
na msamaha na mwishoni, Watoto na Familia.