2013-02-13 14:27:11

Jangwa ni kielelezo cha ukimya, umaskini na mahali pa kukutana na Mungu; ni sehemu ya majaribio na kifo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amekianza kipindi cha Kwaresima ambacho kinakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kwa kusema kwamba, Kwaresima ni hija ya toba na wongofu wa ndani inayomwandaa mwamini kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ni kipindi cha Siku 40 kinachowakumbusha waamini safari ya Waisraeli Jangwani na Siku arobaini ambazo Yesu alijaribiwa na shetani kabla ya kuanza utume na maisha yake ya hadhara.

Jangwa ni mahali pa ukimya panapomwezesha mwamini kukutana na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha; ni mahali pa kufanya maamuzi ya kina kuhusu dira na mwongozo wa maisha; hapa pia ni mahali pa majaribu. Yesu katika kujaribiwa kwake Jangwani kwa siku arobaini, anawaonesha Wafuasi wake jinsi ya kuwa waaminifu katika kutimiza mapenzi ya Mungu, anayewaongoza katika kufikiri na kutenda, hasa katika ulimwengu wa utandawazi.

Mwenyezi Mungu anaendelea kutoa changamoto ya toba na wongofu wa ndani wa hali ya juu kwa mifano ya watu kama vile Pavel Florensky, Etty Hillesum na Dorothy. Ni mwaliko na changamoto kwa waamini pia kufanya toba na wongofu wa ndani. Katika kipindi cha Kwaresima, Yesu anakuja kugonga mlango wa mioyo ya waamini, anawaalika kufungua akili na mioyo yao ili kujikita katika upendo na ukweli.

Baba Mtakatifu anasema, mfano wa Yesu Kristo kuweza kushinda vishawishi iwe ni changamoto ya kukumbatia mapenzi ya Mungu na kuona yote kadiri ya mwanga wa ukweli unao okoa. Kwaresima kiwe ni kipindi cha toba kinachomchangamotisha mwamini kukumbatia utakatifu wa maisha kwa kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Iwe ni fursa ya kudumu katika: sala, kufunga, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kushiriki Sakramenti za Kanisa chemchemi ya neema zote.







All the contents on this site are copyrighted ©.