2013-02-13 07:04:50

Benedikto XVI kung'atuka kutoka madarakani: Ufafanuzi wa kina!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anatarajiwa kuendelea kutekeleza yale yaliyokuwa yamepangwa kwenye ratiba yake kwa kipindi cha Mwezi Februari, 2013. Hii ni pamoja na kuendelea kukutana na Maaskofu waliokuwa wanafanya hija yao ya kitume inayofanyika kila baada ya miaka mitano mjini Vatican, kama nafasi ya kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhusu maisha na utume wa Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuhitimisha Katekesi yake ya kila Jumatano hapo tarehe 27 Februari 2013, inayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu siku ya Alhamisi, tarehe 14 Februari 2013 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Makleri wanaofanya utume na shughuli zao za kichungaji Jimbo kuu la Roma. Katika mkutano huu unaotarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Makleri kutoka Jimbo kuu la Roma, Baba Mtakatifu atawamegea uzoefu na mang’amuzi yake wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; Mtaguso ambao alihudhuria akiwa kama mtaalam mwalikwa, wakati wa ujana wake.

Katika Maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, kama mwanzo wa kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amelazimika kuadhimisha Ibada hii kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kutoa fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema walioonesha utayari wa kuhudhuria Ibada hii inayomkumbusha mwamini kwamba, ni mavumbi na mavumbini atarudi.

Ni mwanzo wa Siku Arobaini za toba na wongofu wa ndani, changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha; Tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti yanayomwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma. Hii itakuwa ni nafasi ya pekee kwa Makardinali, Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini walei kuweza kushiriki kikamilifu katika Ibada kubwa ya hadhara pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ambaye ametangaza nia yake ya kung’atuka kutoka madarakani ifikapo tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku.

Baba Mtakatifu ametulia na anaendelea vyema na maisha yake na wala hakung’atuka kutoka madarakani kwa sababu ya ugonjwa, bali ni kutokana na uzee ambao unaendelea kumwelemea na hivyo kumfanya kutoweza kutekeleza dhamana na utume wake barabara kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Padre Lombardi anasema, hivi karibuni madaktari walimbadilishia beteri ya mashine yake ya moyo, lakini tukio hili halina uhusiano wowote na uamuzi wake wa kung’atuka kutoka madarakani.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alikuwa ameanza kuandika Waraka juu ya Imani, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Waraka huu hautaweza kuwa tayari hadi kufikia tarehe ya kung’atuka kwake madarakani, hivyo kazi hii imesitishwa kwa sasa.

Padre Lombardi anawaalika waamini na hasa wanahabari kusikiliza kwa makini, yale ambayo Baba Mtakatifu anataka kuliambia Kanisa katika kipindi hiki kilichosalia kwake kuwa madarakani. Wazo la kung’atuka lilianza kujitokeza kwa kasi wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Mexico na Cuba, akashuhudia uchovu mkubwa aliokumbatana nao wakati wa safari hii ya kimataifa. Huu ukawa ni mwanzo wa tafakari ya kina kuhusu umri na nguvu alizokuwa nazo katika kukabiliana na majukumu makubwa yanayohitaji nguvu na afya njema.

Watu wanaendelea kuonesha udadisi, baada ya kung’atuka kutoka madarakani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ataitwa nani? Atavaa mavazi gani? Haya ni kati ya masuala yanayoendelea kufanyiwa kazi na Wanasheria wa Kanisa, ikumbukwe kwamba, ni takribani miaka 600 iliyopita tukio kama hili la Papa kung’atuka kutoka madarakani lilipotokea.

Baba Mtakatifu anasema Padre Lombardi anawashukuru waandishi wa habari pamoja na vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii walioshirikiana pamoja naye katika kutekeleza majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Uamuzi wa Baba Mtakatifu kung’atuka kutoka madarakani ni matunda ya tafakari na uchunguzi wa dhamiri mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa, ndiyo maana amebaki kuwa na amani pamoja na utilivu wa ndani.

Padre Lombardi anasema, kuna baadhi ya vyombo vya habari kwa makusudi vilitaka kupotosha ujumbe uliotolewa na Kardinali Dziwisz, Askofu mkuu wa jimbo kuu la Cracovia, kwa kusema kwamba, ujumbe wake wa maandishi unaonesha upendo, heshima na ukarimu kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Pete ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na mhuri wake ni mambo yanayofanyiwa kazi kwa sasa na wanasheria wa Kanisa ili yaweze kutolewa uamuzi wake wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika. Baba Mtakatifu hatausika kwa namna yoyote ile katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati utakapowadia. Sheria za Kanisa zinaonesha kwamba, Kardinali akishafikisha umri wa miaka 80 anang’atuka kutoka katika madaraka na kuachia nafasi hiyo kwa viongozi wengine wa Kanisa ili kuendeleza utume na maisha ya Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayopata umuhimu wa pekee kwa uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama fursa ya kuweza kukutana na kuzungumza na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ndilo lililokuwa wazo lililopelekea kuanzishwa kwa Siku ya Vijana Duniani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Papa anayekuja, ataweza kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatakayofanyika kuanzia tarehe 23 hadi 28 Julai 2013, mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Uwepo wa Mapapa wawili mjini Vatican si taabu wala shida kama wanavyodhani baadhi ya watu. Pengine itakuwa ni fursa kwa Papa mpya kujisikia kuwa na mwombezi karibu yake. Baba Mtakatifu ni mtu wa sala, tafakari na anapenda kuandika, pengine haya ndiyo mambo anayotaka kuyapatia kipaumbele cha pekee wakati atakapokuwa ameng’atuka kutoka madarakani.

Kwa hakika anasema Padre Lombardi, Baba Mtakatifu anaacha mfano na kielelezo makini cha kuiga baada ya mtu kufanya tafakari ya kina mbele ya Mwenyezi Mungu, kuona wajibu wake na kutoa uamuzi wa busara kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa.

Ni mtu anayelifahamu Kanisa kwa mapana na marefu yake, kamwe hakuogopa kukabiliana uso kwa uso na changamoto zilizojitokeza ndani na nje ya Kanisa. Wakati huu watu wengi wanaibuka na mawazo yao! Lakini ukweli anasema Padre Lombardi, Baba Mtakatifu ameamua kung’atuka madarakani kwa utashi na uhuru kamili bila shinikizo lolote.

Baba Mtakatifu amechagua tarehe maalum ya kutangaza uamuzi wake kwa kuzingatia pia Kalenda ya Maadhimisho mbali mbali ya Liturujia na maisha ya Kanisa. Kuna Juma kuu na hatimaye Siku kuu ya Pasaka. Ametamani kwamba, Mkutano wa Makardinali ufanyike wakati wa Kwaresima, ili hatimaye, wakati wa Pasaka, Kanisa liweze kuadhimisha Mafumbo Makuu ya Imani, likiwa na mchungaji wake mkuu.

Ni vyema, ikiwa kama Papa mpya atapata fursa ya kujiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani pamoja na kufunga Mwaka wa Imani. Yote haya ameyafanya kwa kuzingatia uhuru na nguvu ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia hata kufikia uamuzi wa hekima, ujasiri, busara na unyenyekevu mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.