Baraza la Maaskofu Kenya lazindua Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2013
Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya hivi karibuni amezindua
kampeni ya kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 inayoongozwa na kauli mbiu "Napenda
kuona Kenya iliyoungana na yenye amani". Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho
pamoja na Yesu Kristo kwa siku arobaini, ili kujiandaa kusherekea Fumbo la Pasaka.
Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; kufunga na kusali pamoja na kuimwilisha imani
katika matendo.
Kardinali Njue anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi
Mungu, ili kuboresha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Maneno na matendo
yao yawe ni chemchemi ya upendo inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto
ya kukimbilia huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Waamini na wananchi wa Kenya
wakati huu wa mchakato wa uchaguzi mkuu wanaalikwa kuombea amani na utulivu ili maafa
yaliyotokea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008 yasijirudie tena. Hili liwe ni
fundisho kwa wakenya wote kuchuchumilia amani kwa gharama yote.
Kardinali Njue
katika uzinduzi wa Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2013, tukio ambalo limehudhuriwa
na Familia ya Mungu nchini Kenya, anawaalika wananchi wote kuhakikisha kwamba, lugha
ya amani inakuwa ni dira na mwongozo katika maisha yao, kwani huu ndio urithi mkubwa
ambao Yesu mwenyewe amewaachia wanafunzi wake.
Ikumbukwe kwamba, amani ni
zawadi kutoka kwa Mungu, lakini mwanadamu pia ana mchango wake. Watu wajenge utamaduni
wa upendo bila kujali mahali, dini au rangi ya mtu, kwani wote wameumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu.
Amani na utulivu ni vikolezo vya maendeleo ya kiuchumi,
kijamii na kidini, kamwe wananchi wa Kenya wasijitumbukize katika machafuko ya kisiasa
kwani yatawagharimu sana. Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 4 Machi
2013.