Baba Mtakatifu Benedikto XVI ni mfano wa kuigwa katika uamuzi wake wa kung'atuka kutoka
madarakani
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika
na Madagascar, SECAM, ameupongeza uamuzi mzito na wa kishujaa uliofanywa na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita wa kung'atuka kutoka madarakani na kwamba, huu ni mfano
bora na kielelezo cha kuigwa na viongozi wengine duniani.
Ameonesha unyenyekevu
wa hali ya juu kabisa baada ya kuona ukweli kutoka katika undani wake na hatimaye,
kwa utashi na uhuru wake kamili akatamka hadharani kwamba, anang'atuka kutoka madarakani.
Baba Mtakatifu anaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayepaswa kuogopwa zaidi na
kwamba, daima ataendelea kuwapo ili kuwaongoza, kwa kuishi na kutambua kwamba, wao
ni watu wake.
Uamuzi huu iwe ni changamoto kwa viongozi sehemu mbali mbali
za dunia katika utekelezaji wa majukumu yao kwa Jamii kwa kupima uwezo wao na pale
wanapoona kwamba, hawezi kumudu tena, basi wawe na ujasiri wa kung'atuka! Kuna baadhi
ya viongozi wamekaa madarakani kwa kipindi kirefu na watu wanaendelea kuteseka kwa
sababu yao.
Hakuna sababu ya waamini kuingiwa na hofu kwa kung'atuka kwa Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwani Kanisa Katoliki litaendelea kuungana na
kuwa ni kitu kimoja. Kwa hakika ni tukio ambalo limewaacha watu wengi wakiwa wameshikwa
na butwaa baada ya tukio kama hili kufanyika takribani karne sita zilizopita.