2013-02-12 08:02:36

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa unyenyekevu na ujasiri mkuu!


Tamko la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita alilolitoa Jumatatu tarehe 11 Februari 2013 kuhusu kung'atuka kwake kutoka madarakani kutokana na sababu za umri na afya, zimewashtua watu wengi kiasi cha kubaki wameshika tama!

Habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia zinaonesha kutambua mchango wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita pamoja na kuupokea uamuzi wake kwa heshima na taadhima, kwani ni kitendo cha ujasiri, moyo mkuu, unyenyekevu na uwajibikaji. Ni maneno ya Rais Giorgio Napolitano wa Italia, ambaye hivi karibuni walikuwa pamoja kusikiliza Tamasha la muziki lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mkataba wa Laterano.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameonesha mfano na kielelezo cha kuigwa kwa ajili ya mafao ya Kanisa, kwa kuamua kung'atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru kamili. Kanisa Katoliki nchini Italia linamshukuru kwa mchango wake wa hali na mali katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia.

Naye Chancellor Angela Merkel wa Ujerumani anasema amezipokea habari hizi kwa mshtuko mkubwa kiasi cha kuamsha ndani mwake heshima kubwa kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutokana na mikutano yao mjini Roma na alipopata fursa ya kutembelea Ujerumani kunako mwaka 2011. Anakumbuka kwa namna ya pekee hotuba yake kwa Bunge la Shirikisho la Wananchi wa Ujerumani kuhusu dhamana ya wanasiasa katika Jamii: kusimama kidete kulinda na kutetea haki na ukweli. Ni changamoto ambayo imeacha chapa ya kudumu katika maisha yake.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa anasema kwamba, huu ni uamuzi mgumu unaopaswa kuheshimiwa, kwa namna ya pekee kabisa anampongeza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa ujasiri na unyenyekevu wa aina hii.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amemwandikia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ujumbe wa matashi mema na kwamba, watu wengi watakosa hekima na busara yake kama Kiongozi mkuu wa Kanisa. Amejitahidi sana kuhakikisha kwamba, uhusiano kati ya Uingereza na Vatican unaendelea kuimarika.

Askofu mkuu Justin Welby wa Kanisa kuu la Cantebury ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Waanglikani Duniani, anasema, amepokea kwa mshangao mkubwa taarifa za kung'atuka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka madarakani. Kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni dhamana nyeti na yenye heshima ya hali ya juu, inayohitaji kuwa na mwono mpana na ujasiri.

Askofu mkuu Welby anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uwepo wa Papa Benedikto wa kumi na sita aliyejitoa bila ya kujibakiza kuliongoza Kanisa: kwa maneno na matendo yake; kwa sala na huduma za kichungaji, kama mfuasi amini wa Kristo.

Viongozi wengi wanamkumbuka Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa kuendelea kuhamasisha majadiliano ya kidini na kiekumene; huku akisimama kidete kulinda na kutetea: haki, amani, upendo na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuongozwa na kanuni auni. Ni matumaini ya viongozi mbali mbali wa kidini kwamba, Kanisa Katoliki litaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya mafao ya wengi, amani na ustawi wa Jumuiya ya Kimataifa. Wanaendelea kumtakia afya njema, utulivu na amani ya ndani.

Ni uamuzi wa busara unaofumbata hali ya unyenyekevu na ujasiri mkuu, unaoacha chapa ya kudumu kwa watu wengi. Ni Kiongozi aliyeshirikiana na wengine kuhimiza tunu msingi za maisha ya binadamu. Kwa hakika, uamuzi wake unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Amefanya jambo la msingi kwa wakati muafaka.







All the contents on this site are copyrighted ©.