Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa Kipindi cha Kwaresima 2013
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwa ajili ya kukianza kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro, mjini Vatican, majira ya saa 11:00 saa za Ulaya. Uamuzi huu umechukuliwa baada
ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa utashi na uamuzi wake mwenyewe kuamua
kung'atuka kutoka madarakani kuanzia tarehe 28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku.
Imani
ni jibu makini la upendo wa Mungu; upendo ni kielelezo cha maisha katika imani. Upendo
na imani ni chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa bali ni fadhila zinakamilishana,
lakini imani inachukua kipaumbele cha kwanza kuliko upendo, kwa sababu ni zawadi kutoka
kwa Mungu. Kwa ufupi huu ndio muhtasari wa Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013.
Ujumbe wa
Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa Mwaka 2013 unaongozwa
na kauli mbiu “Kuamini katika pendo kunaamsha upendo: tumelifahamu pendo la Mungu
lililoko ndani mwetu”. Kwaresima ya Mwaka huu inakwenda sanjari na Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani, fursa makini ya kutafakari uhusiano uliopo kati ya imani na upendo;
kati ya kumwamini Mungu; kati ya kumwamini Mungu wa Yesu Kristo na upendo ambao kimsingi
ni kazi ya Roho Mtakatifu inayowaongoza waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili
ya Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, imani ni jibu makini la
upendo wa Mungu na kuwa, kuna uhusiano wa dhati kati ya fadhila hizi za kimungu, kama
alivyokwisha bainisha katika Waraka wake wa kichungaji, Mungu ni Upendo. Maisha ya
wakristo wa kwanza yalipata mwelekeo mpya kwa kukutana na kuonja pendo la Kristo katika
hija ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, Mungu ndiye aliyewapenda kwanza, kumbe jibu
ambalo waamini wanamtolea Mungu si amri bali ni kielelezo cha zawadi ya upendo ambao
kwao unamsukuma Mwenyezi mungu kumwendea mwanadamu na hivyo mwanadamu mwenyewe anakuwa
na jukumu la kujishikamanisha na Mungu.
Upendo wa Mungu ni mwaliko kwa mwamini
kujitoa kikamilifu katika akili na utashi wake, kumtambua Mwenyezi Mungu ambaye ni
hai. Huu ni mchakato endelevu katika hija ya maisha ya mwanadamu, lakini zaidi kwa
wahudumu wa upendo wanaopaswa kujishikamanisha na imani kwa Mungu nayejifunua kwa
njia ya Yesu Kristo, akiwaonjesha upendo kwa Mungu na jirani. Kwa njia hii imani inatenda
katika upendo. Dhana ya upendo mkamilifu inapata chimbuko lake kwa kutambua kwanza
kabisa kwamba, mtu anapendwa, anasamehewa na kuhudumiwa na Kristo, aliyejinyenyekesha
kiasi hata cha kuinama na kuwaosha mitume wake miguu; akayamimina maisha yake pale
juu Msalabani ili kuwavuta watu wote katika pendo lake.
Imani aliyo nayo mwamini
kuwa Mwenyezi Mungu amemtoa Mwanaye wa Pekee, inaamsha uhakika kwamba kweli Mungu
ni upendo, unaojionesha kwa kwa njia ya Yesu Kristo aliyetobolewa kwa mkuki ubavuni,
ili kumwonjesha mwanadamu upendo usiokuwa na kifani, unamkirimia nguvu ya kuishi na
kutenda mintarafu upendo unaobubujika kutoka katika kisima cha imani.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, upendo ni kama maisha katika imani,
kwani maisha yote ya Kikristo ni kama jibu muafaka la upendo wa Mungu ambao kimsingi
ni zawadi, inayoonesha hija katika mwanga wa urafiki na Kristo anayetoa maana halisi
ya maisha ya mwamini. Mwenyezi Mungu anapenda kuwavuta watu kwake na kuwapatia mabadiliko
ya ndani, kiasi kwamba, wanaweza kudiriki kusema, si wao wanaoishi, bali Kristo anaishi
ndani wao.
Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2013 anaendelea
kubainisha kwamba, ikiwa kama waamini watamwachia Mungu nafasi katika maisha yao,
wataweza kushiriki kikamilifu katika pendo lake, kiasi kwamba, imani inakuwa tendaji
na Mungu mwenyewe anafanya makao kwa mwamini. Imani inatambua ukweli na kuukumbatia.
Upendo ni mchakato unaomwezesha mwamini kutembea katika ukweli na kwa njia
ya imani, mwamini anajenga urafiki na Kristo; anapokea na kuimwilisha amri ya upendo
pamoja na kuendelea kujisikia kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu wakibeba ndani mwao
tunda la Roho Mtakatifu. Imani inamwezesha mwamini kutambua karama ambazo Mwenyezi
Mungu amemkirimia mwamini na upendo unamsaidia kuzifanya karama hizi ziweze kuzaa
matunda.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya Imani na Mapendo na kwamba si rahisi
kuweza kutenganisha fadhila hizi za Kimungu, lakini ifahamike kwamba, matendo peke
yake hayawezi kuwa mbadala wa imani. Vi vyema kuwa makini kwa kuiwezesha imani kuonekana
katika matendo, kama hija ya kumwendea Mwenyezi Mungu, kwa kumhudumia Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Kanisa la Mwanzo liliweza kustawi kutokana
na kujikita katika huduma kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa
Jamii. Hapa Kanisa linaonesha sura mbili: tafakari na matendo; kama ilivyokuwa katika
maisha ya Maria na Martha; kumbe sura hizi mbili zinapaswa kwenda pamoja katika maisha
na utume wa Kanisa. Mwenyezi Mungu hana budi kupewa kipaumbele cha kwanza na mshikamano
wa kweli wa upendo unapaswa kujikita katika imani.
Kielelezo cha hali ya juu
kabisa cha Upendo ni Uinjilishaji, unaowawezesha Waamini kumegeana Mkate wa Neno la
Mungu kwa kuwasaidia jirani kujenga uhusiano a karibu na Mwenyezi Mungu sanjari na
huduma kwa binadamu. Uinjilishaji wa kina ni kati ya vielelezo vya juu kabisa vya
maendeleo ya binadamu, kama alivyobaini Papa Paulo wa sita. Huu ni ukweli wa upendo
unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ukamwilishwa na kutangazwa; kama utapokelewa
kwa mikono miwili unaweza kuleta maendeleo endelevu kwa kila binadamu.
Upendo
wa Mungu kwa binadamu umefahamika kwa njia ya Utangazaji wa Injili, ukipokelewa kwa
imani thabiti, unawawezesha pia kupenda pendo lenyewe, ili kukua na kukomaa katika
Pendo ili hatimaye, kuwashirikisha wengine ile furaha inayobubujika kutoka katika
Pendo hili. Mwanadamu anakombolewa kwa njia ya Imani, ambayo kimsingi ni zawadi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Ni Mungu mwenyewe anayeanzisha juhudi za kutaka kumkomboa
mwanadamu anayepokea msamaha huu kwa njia ya imani, inayohitaji kwanza kabisa uhuru
na uwajibikaji unaojielekeza katika matendo ya upendo. Haya ni matunda ya imani yanayobubujika
kutoka katika neema ya Mungu na wala si juhudi za mtu binafsi. Imani bila matendo
ni sawa na mti bila matunda; kumbe fadhila hizi mbili ni sawa na chanda na pete, zinafungamana
na kushibana.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema Kipindi cha
Kwaresima ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha
Neno la Mungu katik uhalisia wa maisha; kushiriki Sakramenti za Kanisa pamoja na kutenda
matendo ya huruma kwa Mungu na jirani kwa njia ya kufunga, matendo ya toba na kutoa
sadaka. Lakini ikumbukwe kwamba, Imani inachukua kipaumbele cha pekee kuliko upendo,
kwani Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba fadhila zote mbili ni kazi ya Roho
Mtakatifu.
Imani ni zawadi na jibu makini linalomwezesha mwamini kuufahamu
ukweli juu ya Kristo kuwa ni Upendo uliomwilishwa na kusulubishwa; upendo mkamilifu
unaojikita katika mapenzi ya Mungu na huruma isiyokuwa na kifani kwa jirani. Imani
inajikita katika moyo na akili ya mwamini, inayomwezesha kupata ushindi dhidi ya ubaya
na kifo.
Imani inamsukuma mwamini kutumainia kwamba, siku moja upendo wa Kristo
utaweza kufikia utimilifu wake. Upendo unamwezesha mwamini kuingia katika mahusiano
na Mungu aliyejionesha kwa njia ya Yesu Kristo, kiasi cha mwamini kujitoa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Sakramenti ya
Ubatizo ambayo ni kielelezo cha imani na sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo
cha upendo. Sakramenti ya Ubatizo inatangulia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, lakini
zote ni muhimu katika utimilifu wa hija ya maisha ya Mkristo. Imani iwawezesha waamini
kumpenda Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha
Ujumbe wake wa Kwaresima kwa kuwakumbusha kwamba, Kipindi cha Kwaresima kinawawezesha
kujiandaa kikamilifu katika kusherehekea Fumbo la Pasaka:Mateso yanayojionesha kwa
njia ya Msalaba na Ufufuko unaodhihirisha kwamba, upendo wa Mungu umeukomboa ulimwengu;
changamoto ya kuishi kikamilifu imani na mapendo kwa Mungu na jirani.