Mkutano wa Dekania ya Makardinali kwa kama unavyojulikana na wengi "Conclave" utakaokutana
mwanzoni mwa Mwezi Machi mwaka huu ili kumchagua Papa mwingine baada ya Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita kung'atuka madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013 utaongozwa
na Katiba iliyotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili "Universi Dominici
Gregis".
Kardinali Camerlengo Tarcisio Bertone, aliyeteuliwa na Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita hapo tarehe 4 Aprili 2007 atakuwa ni kiongozi
mkuu katika kipindi hiki cha mpito.
Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa
kura kwa sasa kutoka Barani Ulaya ni Makardinali 61, Amerika ya Kusini wako 19, Amerika
ya Kaskazini kuna Makardinali 14, kutoka Barani Afrika kuna Makardinali 11, Bara la
Asia ni Makardinali 11na kuna Kardinali mmoja kutoka Oceania. Idadi ya Makardinali
wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura inaweza kubadilika kadiri ya tarehe za kuzaliwa
Makardinali. Kwa mfano, Kardinali Walter Kasper, tarehe 5 machi 2013 atasherehekea
miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, kuna Makardinali
wengi kutoka Italia, ambayo ina Makardinali 21. Makardinali 67 wenye haki ya kupiga
na kupigiwa kura waliteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika kipindi
cha uongozi wake. Makardinali 117 watakaokuwa na dhamana ya kumchagua Papa Mpya watalazimika
kuishi ndani ya Vatican, nje kidogo ya Kikanisa cha Sistina, mahali ambapo mchakato
wa uchaguzi wa Papa mpya utakuwa unaendelea.
Wakati wote huu, Makardinali
wataishi ndani ya Vatican na hakuna atakayeruhusiwa kukutana nao wakati wote wa mkutano
wa kumchagua Papa wakati wanatoka au kurudi kutoka katika Kikanisa cha Sitina. Mawasiliano
yote na watu wa nje yamazuiliwa.
Uchaguzi wa Papa utakapokamilika, ishala
ya moshi mweupe itatolewa na hatimaye, Papa Mpya kutangazwa. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican, itakuwa nawe sambamba ili kukujuvya yanayojiri wakati wote huu.