Kanisa limelipokea Tamko la Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa mshangao mkubwa!
Kardinalo Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumatatu tarehe 11 Februari 2013 kwa
niaba ya Makardinali wenzake amemwambia Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwamba,
wamepokea habari za kung'atuka kwake madarakani kwa mshangao mkubwa! Ni tamko linaloonesha
upendo mkuu kwa Kanisa la Mungu.
Makardinali wataendelea kumwonesha mshikamano
na ushirikiano wa dhati hasa wakati huu baada ya kufanya maamuzi mazito kwa ajili
ya mafao na ustawi wa Kanisa baada ya kuliongoza Kanisa Katoliki kwa takribani miaka
8. Ilikuwa ni tarehe 19 Aprili 2005 alipokubali kubeba dhamana ya uongozi wa Kanisa
Katoliki, akajiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, akifuata nyayo za
watangulizi wake 265 waliowahi kuliongoza Kanisa Katoliki tangu Mtakatifu Petro, yapata
miaka elfu mbili iliyopita.
Kardinali Sodano anabainisha kwamba, kabla ya tarehe
28 Februari 2013, saa 2:00 Usiku, watapata nafasi ya kutoa heshima na shukrani zao
za dhati, kama ambavyo watafanya viongozi wa Kanisa, Waamini na Watu wenye mapenzi
mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi hiki cha mpito, Kanisa bado
litaendelea kumsikiliza Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika mahubiri
yake Jumatano ya Majivu, Mama Kanisa anapokianza kipindi cha Kwaresima; kwenye Katekesi
zake Jumatano, Mkutano pamoja na Makleri wa Jimbo kuu la Roma pamoja na tafakari zake
wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana.