2013-02-11 11:21:02

Ujumbe wa Bikira Maria wa Lourdes: wongofu wa ndani, sala na matendo ya huruma


Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani ni fursa makini ya kusali, kushirikishana na kutolea mateso kwa ajili ya mafao ya Kanisa na changamoto ya kuendelea kuiangalia ile sura ya Kristo mteswa miongoni mwa wagonjwa na wote wanaoteseka kimwili na kiroho.

Bikira Maria ni mwombezi wa wote wanaomkimbilia katika shida na magumu ya maisha; watu wanaojitahidi kutubu na kuongoka, hao kwa hakika wanaonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao, kama inavyojionesha kwa baadhi ya waamini wanaofanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, kwenye Kanisa kuu la Chennai na kama sehemu ya uzinduzi wa Seminari ya Kitaifa kwa ajili ya majiundo ya waamini walei nchini India.. Ujumbe wa Bikira Maria wa Lourdes, daima umekuwa ukisisitiza juu ya wongofu wa ndani, sala na matendo ya huruma. Hapa kumekuwa ni chem chemi ya neema, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia umuhimu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao pamoja na matumizi makini ya karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Walei wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara ili waweze kuwa ni mashahidi wa Kristo na Kanisa lake.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa makini kwa waamini kutambua na kutekeleza wito na dhamana yao ndani ya Kanisa. Fadhila ya imani, matumaini na mapendo zijioneshe miongoni mwa waamini; daima wakijitahidi kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, ili kuwasaidia watu kujenga uhusiano na mshikamano wa dhati na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Mwaka wa Imani ukoleze maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yanayofikia kilele chake katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wajikite katika maisha ya sala na ushuhuda wa imani tendaji. Waamini walei wajishughulishe kikamilifu katika medani mbali mbali za maisha ya watu.

Vyama vya kitume, viwe ni cheche za majiundo, urithishaji wa imani pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kichungaji inayotolewa na Makanisa mahalia. Waamini wajitahidi kukuza na kudumisha moyo na ari ya kimissionari, tayari kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.