Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia baada ya mkutano
Taarifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mkutano wake uliohitimishwa hivi
karibuni, wanamwona Yesu kuwa ndiye Msamaria mwema, changamoto kwa Kanisa kuendelea
kuwa ni Msamaria mwema kwa wote wanaoteseka na kutaabika kiroho na kimwili.
Maaskofu wanaonesha
mshikamano wao wa dhati na kundi kubwa la vijana ambao kwa sasa halina fursa za ajira,
pamoja na familia ambazo zinaendelea kuteseka kutokana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa; changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya waamini kushirikishana fadhila ya
upendo na mshikamano wa dhati.
Wanasiasa wajikite katika mchakato utakaoibua
mbinu mkakati wa maboresho ya uchumi na hali ya wananchi wengi wanaoendelea kuogelea
katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato. Parokia mbali mbali nchini Italia, ziendelee
kujenga na kuimarisha ari na mwamko wa kimissionari, kwa kushirikishana fadhila ya
imani.
Ni mwaliko kwa wadau mbali mbali wa Uinjilishaji, kujikita katika ufundishaji
makini wa Katekesi, itakayowasaidia waamini kukiri, kuadhimisha, kuimwilisha, kuisali
na hatimaye kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha. Iwe ni fursa kugundua utambulisho
wao wa Kikristo na mwaliko wa kumfuasa Kristo kwa moyo na ari kubwa zaidi hasa wakati
huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.
Maaskofu wameangalia na kubainisha
mikakati itakayotumika kwa ajili ya kuwaandaa vijana wanaotaka kumfuasa Kristo katika
maisha ya Kipadre; Umuhimu wa kuwa na majiundo endelevu ya kipadre pamoja na kuendelea
kuhimiza umuhimu wa vituo vya vijana Parokiani kama mahali pa majiundo ya Kikristo,
bila kusahau huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, limeaanza mchakato wa maandalizi
ya Kongamano la Kitaifa litakalofanyika Jimboni Firenze kunako mwaka 2015. Wanaendelea
kuunga mkono jitihada za vyama vya kitume vinavyotaka uhuru kamili katika masuala
ya elimu na maisha ya binadamu, yanayopaswa kulindwa na kuthaminiwa tangu pale mtoto
anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake.
Maaskofu wanasema, wataendelea kuwa
ni sauti ya kinabii miongoni mwa maskini na wahitaji, kamwe hawatanyamaza bali wataendelea
kuwa ni Wasamaria wema, wanaosikiliza kwa makini; wanaoelimisha na kusaidia. Ubinafsi
wa kukithiri ni kati ya mambo makubwa yanayosababisha myumbo wa kiuchumi, kimaadili
na kiutu. Kama viongozi wa Kanisa, wataendelea kumtangaza Yesu Kristo aliyeteswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kiini cha imani yao.
Ni matumaini ya
watu wengi kwamba, kwa njia ya Kanisa, wanaweza kujenga na kuimarisha mahusiano yao
ya Kijamii, kiasi hata cha kuweza kushirikisha utajiri na maisha yao ya kiimani. Hii
ni changamoto kwa Parokia kuendelea kuwa kweli ni mahali pa kukuza na kudumisha ari
na moyo wa kimissionari.
Mikakati ya kichungaji kuhusu familia ipewe kipaumbele
cha kwanza kwani Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; mahali ambapo watu wanaonja na
kumegeana upendo na mshikamano wa dhati, kila mtu akiwajibika barabara. Jamii inapaswa
kuwekeza katika familia kama njia ya kudhibiti athari za myumbo wa uchumi kimataifa
nchini Italia.