Mwaka wa Imani ujioneshe kwa namna ya pekee kwa njia ya Imani tendaji!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu
katika ziara yake ya kikazi nchini India, Jumapili tarehe 10 Februari 2013 alitembelea
Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Afya Njema, yaliyoko Vailankanni, India na
kusema kwamba, kwa hakika Bikira Maria ni chombo cha upendo wa Mungu, hasa wakati
huu Madhabahu haya yanapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu yalipojengwa sanjari
na Mwaka wa Imani.
Amewapatia salam na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita. Makanisa yote yaliyowekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira
Maria ni kielelezo cha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu kama alivyotangazwa na
Mtaguso wa Efeso kunako mwaka 431. Yesu mwenyewe aliwaonesha mitume wake Mama yao
ambaye wangepaswa kumtunza, changamoto ya kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji Mpya
sehemu mbali mbali za dunia. Miaka 50 tangu Madhabahu haya yalipoanzishwa, yamekuwa
ni kielelezo cha imani na upendo kwa Bikira Maria.
Bikira Maria ni Mama wa
Mungu na wa Kanisa, Mfariji wa wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini, hasa kwa
wale wanaomtumikia na kumpenda Mwanaye wa Pekee. Huu ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo
kwa makini pamoja na kuendelea kumjifunza Kristo kutoka katika shule ya Bikira Maria;
daima wakijitahidi kutekeleza kile anacho waamuru kutenda; huku wakijitahidi kuchuchumilia
wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Bikira Maria ni kielelezo cha mtu
wa sala anayewaombea watu mahitaji yao ya msingi pamoja na neema. Muujiza wa arusi
ya Kana ulipania kuwaimarisha wafuasi wake katika imani, ili kubadili maisha yao mintarafu
mpango wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, iwe ni fursa ya kujibidisha kuifahamu
vyema imani kwa Kristo na Kanisa lake.
Hii ndiyo ile hija ya imani na matumaini
aliyofanya Bikira Maria tangu alipopashwa habari kwamba, atakuwa Mama wa Mungu, alipomtembelea
binamu yake Elizabeth na walipolazimika kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto
Yesu, hadi pale aliposimama chini ya Msalaba na baadaye kupokea Zawadi ya Roho Mtakatifu.
Mwaka wa Imani ujioneshe kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Kardinali Fernando
Filoni anawaalika waamini nchini India katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wajibidishe
zaidi na zaidi katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwa ari na kasi kubwa zaidi. Kardinali
Filoni pia alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu katoliki
India.