2013-02-11 09:37:33

Bikira Maria anapenda kuwa karibu zaidi na: Maskini, Wagonjwa na Wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita mara baada ya tafakari ya Sala ya Mchana, Jumapili iliyopita, tarehe 10 Februari 2013 aliwakumbuka kwa namna ya pekee wananchi wanaoishi Mashariki ya Mbali walipokuwa wanaadhimisha Mwaka Mpya. Amani, utulivu na shukrani ni tunu msingi zinazokumbukwa na wananchi wanapoadhimisha Siku kuu hii, kama nyenzo muhimu ya ujenzi wa: Familia, Jamii na Taifa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, tunu hizi zitaweza kuwasaidia wananchi wa Mashariki ya Mbali kupata maisha ya furaha na maendeleo endelevu. Anawaalika Waamini wa Kanisa Katoliki katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waongozwe na hekima ya Kristo.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anakumbusha kwamba, kila Mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, ambayo kwa mwaka huu yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Altotting nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu anasema kwa njia ya sala na sadaka yake, yuko pamoja na wagonjwa wote na anajiunga kiroho na wote wanaoadhimisha Siku hii huko Ujerumani.

Bikira Maria Mama wa Mungu mjini Lourdes, Ufaransa amejionesha kwa Mtakatifu Bernadetha Soubirous kuwa fukara; akamwonesha chemchemi ya faraja, ambayo imewaonjesha huruma ya Mungu kwa kuwaponya magonjwa yao. Bikira Maria anapenda kuwa karibu zaidi na maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kwa pamoja waweze kuanza hija ya imani kumwendea Yesu Kristo. Baba Mtakatifu anawaweka wagonjwa wote chini ya usimamizi, faraja na maombezi ya Bikira Maria.








All the contents on this site are copyrighted ©.