2013-02-09 13:56:55

Kongamano la Kimataifa kuchambua mawasiliano katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na Siku ya Vijana Duniani


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Brazil kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013 ni kati ya changamoto zitakazofanyiwa kazi kwenye Kongamano la Mawasiliano ya Jamii Kimataifa, litakalofanyika kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 10 Aprili 2013, kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Chile.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano amealikwa kama mgeni rasmi katika maadhimisho haya, ili kushirikisha changamoto za mawasiliano ya Jamii katika azma ya Uinjilishaji mpya, changamoto inayovaliwa njuga na Mama Kanisa wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mkazo ni kuangalia utume wa Mama Kanisa kwa vijana sanjari na changamoto za mawasiliano ya Jamii baada ya kipindi cha miaka 25 tangu Siku ya Vijana Duniani ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza Amerika ya Kusini.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita; Uinjilishaji Mpya na Utandawazi na Maendeleo ya Sayansi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni mambo yatakayochochea majadiliano wakati wa kongamano hili la kimataifa. Wajumbe pia watapata fursa ya kuangalia na kujadili njia za mawasiliano ya asili kama vyombo vya mawasiliano, ili kuleta mwamko na ari mpya katika hija ya imani miongoni mwa vijana.

Kwa namna ya pekee, wajumbe hawa wataangalia na kupembua mikakati inayoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika kuhakikisha kwamba, linakuwa na matumizi bora zaidi ya mitandao ya Kijamii, ambalo kwa sasa limekuwa ni "Kijiwe cha Vijana wa Kizazi Kipya".







All the contents on this site are copyrighted ©.