Caritas MONA, kukutana ili kujadili mikakati ya kuwasaidia wakimbizi kutoka Mashariki
ya Kati na Afrika ya Kaskazini
Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Mashariki ya Kati, na Kaskazini
mwa Afrika, Caritas MONA, linalojumuisha mashirika 17, kuanzia tarehe 20 hadi 22 Februari,
2013 litakuwa na mkutano wake mkuu, utakaofanyika mjini Amman, nchini Yordani. Tatizo
la wakimbizi Mashariki ya Kati ni kati ya ajenda kuu zitakazofanyiwa kazi na wajumbe
41 waliokwisha thibitisha kwamba, watashiriki.
Kardinali Robert Sarah, Rais
wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anatarajiwa
pia kushiriki katika mkutano huu. Hapo tarehe 19 Februari, Kardinali Sarah atatembelea
Familia za wakimbizi kutoka Syria ili kushiriki pamoja nao shida na mahangaiko yao
ya ndani. Wajumbe wa mkutano huu wanatarajiwa pia kukutana na Mfalme Abdallah wa Pili
wa Yordan.
Wajumbe pia watapembua kwa kina na mapana mikakati ya shughuli za
kichungaji na utekelezaji wake katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum katika maeneo yao. Mateso na mahangaiko ya wakimbizi kutoka Syria
ni changamoto kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.