2013-02-08 07:33:31

TANZIA: Askofu Thomas Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha, Kanisa la Kiluteri la Kiinjili Tanzania amefariki dunia


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Februari 7, 2013, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Mkuu Dkt. Alex Malasusa kuombeleza kifo cha Askofu Thomas O. Laizer wa Jimbo la Kaskazini Kati Arusha la KKKT aliyeaga dunia tarehe 7 Februari 2013.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Askofu Mkuu Malasusa: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Askofu Thomas Laizer ambaye nimejulishwa kuwa ameaga dunia muda mfupi uliopita, jioni ya leo, katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, Arusha.”

“Askofu Thomas Laizer ametutoka lakini tutaendelea kumkumbuka kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi wa kiroho wa Watanzania na ambaye wakati huo alitafuta namna bora zaidi ya kuwatumikia waumini wake. Daima atakumbukwa kama kiongozi ambaye alitumia vipaji vyake vyote kuwatumikia waumini wake na wote waliokuwa chini yake.”

Ameongeza Rais kikwete: “Kufuatia msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Baba Askofu Mkuu Alex Malasusa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kukupa pole ya msiba huu na kupitia kwako kuwapa pole nyingi maaskofu na viongozi wenzako katika KKKT pamoja na waumini wote wa Kanisa kwa kuondokewa na kiongozi mwenzao na muumini mwenzao.”

Aidha, Rais Kikwete ameongeza, “Pia kupitia kwako Baba Askofu Mkuu, natuma salamu nyingi za moyoni mwangu kwa familia na wana-ndugu wa Marehemu Thomas Laizer. Naungana nao katika kuomboleza. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na Baba, Babu na mhimili wa familia. Nawaombea subira ili waweze kuvuka kipindi hiki kwa sababu yote ni Mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Thomas Laizer. Amen.”









All the contents on this site are copyrighted ©.