2013-02-08 08:37:16

Kanisa Katoliki Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa wa huduma katika sekta ya afya!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika anabainisha kwamba, Kanisa tangu awali limekuwa likijihusisha na utoaji wa huduma ya afya kwa kuendeleza lile agizo la Kristo kwa wafuasi wake la kuponya magonjwa na udhaifu wa kila aina. RealAudioMP3

Hii ni changamoto kwa Taasisi za Kanisa zinazotoa huduma ya afya pamoja na wahudumu wa sekta ya afya kujitahidi kuona kwamba, kila mgonjwa ni kiungo kinachoteseka cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wahudumu wa sekta ya afya wanachangamotishwa na Baba Mtakatifu kuwaonjesha wagonjwa ule upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Yesu mwenyewe, kwa ajili ya watu wenye shida. Anawataka kusimama imara katika imani na matumaini na kamwe wasife moyo wala kukata tamaa.

Taasisi za huduma ya afya hazina budi kuongozwa kufuatana na kanuni maadili za Kanisa, daima zikijitahidi kuenzi Injili ya uhai; daima ziwakumbushe wahudumu wa sekta ya afya na wagonjwa kwamba, Mungu peke yake ndiye Bwana wa uhai na mauti. Ndiyo changamoto ambayo Kanisa Katoliki Tanzania limeendeleza hadi wakati huu linapomshukuru Mungu kwa kumwimbia utenzi wa shukrani kwa miaka 150 ya Uinjilishaji wa kina, ambao umejionesha kwa namna ya pekee katika huduma, hususan kwenye sekta ya Afya na Elimu.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania anabainisha kwamba, huduma kwa wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni sehemu ya wito na utume wa Kanisa. Kanisa Katoliki nchini Tanzania, licha ya wakati fulani Serikali kutaifisha Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya vilivyokuwa vinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Tanzania, limeendelea kuwekeza katika sekta ya afya, kama lengo la kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeendelea kuratibu huduma hizi katika Majimbo na Parokia mbali mbali, ili kuhakikisha kwamba, zinakwenda kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki, kwa kulenga kudumisha zawadi ya uhai, utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa pia limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma ya maji safi na salama sehemu mbali mbali za Tanzania na kwamba, limeendelea kuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo endelevu nchini Tanzania.

Askofu Mkuu Lebulu anasema kwamba, kwa hakika katika kipindi cha Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa Katoliki limepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa wito na utume wake miongoni mwa Watanzania na kwa sasa wanayo haki ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani na hasa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.