Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la Wahudumu Katika Sekta ya
Afya anasema, Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2013 yanaongozwa na
kauli mbiu “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”. Kilele cha maadhimisho haya ni
hapo tarehe 11 Februari 2013 kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Hii ni siku
iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 13 Mei 1992, kama sehemu
ya utambuzi wa dhamana na wajibu wa Mama Kanisa katika kuendeleza mchakato wa huduma
kwa wagonjwa, utume ambao ulianzishwa na Kristo mwenyewe, kama harakati za kumkomboa
mtu mzima: kiroho na kimwili. Siku hii inalenga pamoja na mambo mengine, kuonesha
mshikamano wa dhati na wagonjwa pamoja na wale wote wanaoteseka kiroho na kimwili,
ili wanasiasa, watunga sera na wadau mbali mbali waweze kuchangia kwa hali na mali
katika maboresho ya huduma ya afya, kwa kukumbatia Injili ya Uhai. Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuitambua
ile sura ya Yesu Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti miongoni mwa wagonjwa wanaokutana
nao katika familia, hospitali na nyumba maalum za wagonjwa na wazee. Maadhimisho
ya Siku ya 21 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2013 yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira
Maria wa Altotting, Ujerumani. Ni fursa kwa wataalam mbali mbali kujadili umuhimu
wa kuwahudumia wagonjwa kiroho na kimwili pamoja na kutembelea wagonjwa waliolazwa
katika Hospitali mbali mbali nchini Ujerumani. Haya ni matendo ambayo yanaweza pia
kutekelezwa na waamini katika Majimbo na Parokia zao, kama sehemu ya Maadhimisho ya
Siku ya Wagonjwa Duniani. Askofu mkuu Zimowski anasema, katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wote
wenye mapenzi mema, kuiga mfano wa Msamaria mwema, aliyeona, akaguswa na taabu pamoja
na mahangaiko ya yule mgonjwa, kiasi cha kumshughulikia. Yesu Kristo ni kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha Msamaria mwema, aliyejitwalia hali ya ubinadamu, ili kumganga
mwanadamu na ile divai ya huruma ya Mungu, inayoendelezwa na Mama Kanisa kwa njia
ya Sakramenti ya Upatanisho. Ni changamoto na mwaliko wa kujenga na kuimarisha mshikamano
wa upendo na wote wanaoteseka kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa
Duniani iwe ni fursa ya kujenga utamaduni wa kusali kwa ajili pamoja na wagonjwa,
ili wagonjwa waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kutekeleza wajibu
wao kwa kuzingatia kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; wajitahidi kukumbatia
na kuenzi Injili ya Uhai na kwamba, dhamana yao kubwa ni kulinda na kutetea uhai wa
binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo! Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, iwasukume
kuwa ni Wasamaria wema, wanaoguswa na mateso ya wagonjwa wanaowahudumia kila siku.