2013-02-07 09:04:41

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya Bwana Chokri Belaid


Kamishina wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amelaani mauaji ya Bwana Chokri Belaid, Katibu mkuu wa Chama cha Democratic Patriots Movement ambaye alikuwa ni kati ya wanaharakati wakuu wa upinzani nchini Tunisia, kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu pamoja na kuendeleza mchakato wa demokrasia nchini mwake.

Bi Pillay anasema, mauaji yake ni pigo kubwa katika kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli nchini Tunisia, ambayo kwa sasa imeingia katika cheche za machafuko makubwa kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Bwana Chokri Belaid alipigwa risasi Jumatano, tarehe 6 Februari 2013 alipokuwa anatoka nyumbani kwake kuelekea kazini.

Kaminisha wa haki za binadamu anawaalika wananchi na wapeneda amani nchini Tunisia, kuungana pamoja kupinga siasa za mauaji zinazolenga kuwafumba mdomo wapinzani katika harakati za kutetea na kulinda haki msingi za binadamu. Marehemu Belaid ataendelea kukumbukwa kutoka na mchango wake katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.