TANZIA: Askofu Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania amefariki dunia
Askofu mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania amefariki dunia
Alhamisi, tarehe 7 Februari 2013 wakati akiwa anaendelea na matibabu Nairobi. Habari
zimethibitishwa na Padre Anthony Makunde, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania. Naye Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki Moshi katika taarifa yake anasema,
Jimbo Katoliki Moshi linaendelea kufanya utaratibu wa mipango ya mazishi na ikikamilika,
taarifa rasmi itaweza kutolewa. Marehemu Askofu Msarikie alizaliwa kunako mwezi
Septemba 1931, Makundi, Kirua Vunjo Moshi, Kilimanjaro. Baada ya masomo na majiundo
yake ya Kipadre, kunako tarehe 8 Agosti 1961 akapadrishwa. Tarehe 21 Machi 1986 akateuliwa
na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Moshi. Akawekwa
wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi tarehe Mosi Mei 1986. Baada ya kuwaongoza,
kuwafundisha na kuwatakatifuza waamini wa Jimbo Katoliki Moshi, kama kiongozi wao
mkuu, tarehe 21 Novemba 2007, akang’atuka kutoka Madarakani.