2013-02-07 10:59:33

Rais Obama kutembelea Israeli mwezi Machi, 2013


Rais Barack Obama wa Marekani kwa mara ya kwanza kama Rais wa Marekani anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Israeli, mwishoni mwa Mwezi Machi 2013. Kati ya mambo anayotarajiwa kuzungumza pamoja na mwenyeji wake ni suala la Iran, Syria na umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya Israeli na Palestina. Hayo yamebainishwa na Bwana Daniel Shapiro, Balozi wa Marekani nchini Israeli, hapo tarehe 6 Februari 2013.

Hizi ni juhudi za Rais Obama kuendeleza majadiliano na Iran kuhusu silaha za kinyuklia zinazomilikiwa na Iran, ambazo zimekuwa ni tishio kwa amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuendeleza juhudi za kidiplomasia, shinikizo la kiuchumi pamoja na Iran kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, ikiwa kama njia nyingine zote zitashindikana.

Kuhusu Syria, bado kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatumia kila njia inayowezekana ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kivita unaoendelea nchini Syria na madhara yake kwa sasa ni makubwa. Ziara hii ya kikzazi ya siku tatu, itamwezesha pia Rais Obama kukutana na viongozi wa Palestina na Jordan.







All the contents on this site are copyrighted ©.