2013-02-07 13:29:46

Mshikamano wa upendo na watoto wa Kijiji cha Matumaini Dodoma


Mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania Mama Tunu Pinda ametoa zawadi mbalimbali kwa watoto zaidi ya 160 wanaoishi kwenye kijiji cha Matumaini ambacho kinalea watoto yatima eneo la Kisasa, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Mama Pinda alizuru kijiji hicho kinacholea watoto yatima Alhamisi, Februari 7, 2013 akiwa amefuatana na viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo, Bi. Salome Kiwaya.


Akizungumza na watoto wa kituo hicho, Mama Pinda alisema ameamua kuwatembelea watoto hao ili kuwasalimia na kuwatakia heri ya mwaka mpya 2013.

Mkurugenzi wa kijiji hicho, Sista Rosalia Gargiulo wa Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Yesu alimshukuru Mama Pinda na viongozi wengine alioambatana nao kwa upendo wao na kwa kutoa muda wao kuamua kuwatembelea na kuwafariji watoto hao.

Meneja mradi wa kijiji hicho ambacho pia kinalea watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, Padre Vincent Boselli, C.PP.S, alisema Kijiji hicho kilianzishwa mwaka 2002 kikiwa na watoto watatu na sasa hivi kina watoto 161 wanaolelewa kituoni hapo kwa mtindo wa familia kwenye nyumba 14 ambazo zina baba na mama wa kujitolea.

Zawadi hizo zenye thamani ya sh. milioni 1.1 ni mbuzi wawili, mchele (kg. 50), sukari (kg. 25), unga wa mahindi (kg. 50), mafuta ya kupikia (lita 40), katoni moja ya sabuni za miche, ndoo moja ya sabuni ya unga, madaftari dazeni tisa, penseli 100, vichongeo 100 na rula 100. Nyingine ni biskuti (katoni tatu), pipi (pakiti nne), juisi (katoni tisa) na khanga.









All the contents on this site are copyrighted ©.